9.8 C
New York

Maandamano Ufaransa; zaidi ya watu 1,000 wakamatwa

Published:

PARIS, Ufaransa

MAAFISA wa usalama nchini Ufaransa wamesema wamewakamata zaidi ya watu 1,000 baada ya mamia ya maelfu ya wananchi kushiriki maandamano yaliyoambatana na makabiliano kati ya waandamanaji na polisi katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.

Ingawa maandamano mengi yalifanyika kwa amani kwa muda mrefu wa siku, polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi na magari ya kunyunyizia maji kuwatawanya waandamanaji katika miji kadhaa, ikiwemo Paris.

Katika mji wa Marseille, baadhi ya vizuizi vya barabarani vilichomwa moto, huku Bordeaux ikishuhudia watu wakivunja mbao zilizokuwa zimefunika duka moja.

Hata hivyo, maafisa wa usalama wamesema walifanikiwa kudhibiti ghasia na uporaji kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na machafuko yaliyotokea mwishoni mwa wiki iliyopita, yaliyotajwa kuwa miongoni mwa matukio mabaya zaidi ya kuvurugika kwa amani katika historia ya kisasa ya Ufaransa.

Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ufaransa, takriban watu 410,000 walishiriki maandamano hayo, huku vyama vya wafanyakazi vikikadiria idadi hiyo kufikia karibu 800,000.

Mapema wiki hii, Rais Emmanuel Macron alitangaza kuwa maandamano yatakayoruhusiwa ni yale yaliyoandaliwa na vyama vya wafanyakazi vinavyotambuliwa rasmi.

Katika siku za hivi karibuni, mamia ya watu wamehukumiwa vifungo vya jela kwa makosa yanayohusisha uharibifu wa mali, uchomaji moto na uporaji, baada ya kesi zao kusikilizwa kupitia taratibu za haraka za mahakama.

Related articles

Recent articles