LONDON, Uingereza
MSHINDI wa tuzo ya Ballon d’Or kwa mwaka huu [2026] atajulikana kesho Oktoba 26, 2026, huku ushindani ukiwa mkali kwa nyota wawili, Lamine Yamal wa Barcelona na Harry Kane anayekipiga Bayern Munich.
Kane alikuwa wa moto msimu uliopita [2025-26], ambapo alifunga mabao 61 katika mechi 51 alizocheza akiwa na Bayern. Kati ya hayo, mabao 36 yalimpa tuzo ya Mfungaji Bora wa Bundesliga na ile ya Ligi zote za Ulaya. Alitwaa mataji mawili ya ndani [Bundesliga na DFB-Pokal].
Katika ngazi ya timu ya taifa, Kane akiwa nahodha wa England aliifungia mabao sita kwenye fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu. ‘Three Lions’ ilishika nafasi ya tatu.
Yamal, licha ya umri wake mdogo wa miaka 19, aliiongoza Barcelona kutetea ubingwa wa La Liga msimu uliopita. Pia, alitwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa msimu huo wa 2025-26 akiwa na mabao 16 na asisti 12.
Kwa timu yake ya Taifa ya Hispania, aliiongoza kutwaa Kombe la Dunia mwaka huu na mwaka 2025 alishika nafasi ya pili wakati Ousmane Dembele anatwaa tuzo ya Ballon d’Or.
Endapo atampiku Kane na kutwaa Ballon d’Or, Yamal ataweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kushinda tuzo hiyo. Ataivunja rekodi anayoshikilia Ronaldo Nazario, ambaye alibeba Ballon d’Or akiwa na miaka 21 mwaka 1997.


