23.5 C
New York

Auawa kwa panga akiwa kikao cha usuluhishi wa familia

Published:

Na Malima Lubasha, Gazetini

SERENGETI. MKAZI wa Kitongoji cha Kwirambo, Kijiji cha Bonchugu, Tarafa ya Rogoro, Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Magige Ryoba (38), amefariki dunia baada ya kukatwa shingo kwa panga, akidaiwa kushambuliwa na mdogo wake wakati wa kikao cha familia cha usuluhishi.

Akizungumza na gazeti hili, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo, amesema hadi wakati huo ofisi yake ilikuwa haijapokea taarifa rasmi kuhusu tukio hilo la mauaji.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Simion Gagiri, amesema tukio hilo lilitokea Septemba 27, 2026, majira ya saa 3:00 usiku katika Kitongoji cha Kilimo B, mpakani mwa Vijiji vya Rwamchanga na Bonchugu, nyumbani kwa mtuhumiwa ambaye amemtaja kuwa ni Makuri Ryoba (20).

Gagiri amesema kabla ya tukio hilo, Bhoke Galu, ambaye ni mama mzazi wa Makuri, alikuwa akilalamikia mwenendo wa kijana wake, akidai kuwa alikuwa katika uhusiano wa kimapenzi na mwanamke mmoja mjane.

Amesema kutokana na hali hiyo, Bhoke alimwomba Magige, ambaye ni kaka mkubwa wa Makuri, kufika nyumbani ili kumshauri mdogo wake kuacha mwenendo huo.

“Bhoke Galu, mama mzazi wa Makuri, alikuwa akilalamikia mahusiano ya kimapenzi ya mtoto wake na mwanamke mjane, akisema uhusiano huo unampotezea muda kijana huyo. Hivyo, alimtaka marehemu Magige kufika nyumbani kumshauri ndugu yake kuacha mwenendo huo. Mtuhumiwa naye alikuwa akilalamikia Magige na mama yake kwamba wanamsema,” amesema Gagiri.

Amesema Magige aliitikia wito huo na kufika katika Kitongoji cha Kilimo B, Kijiji cha Rwamchanga, kwa ajili ya kumshauri mdogo wake.

Hata hivyo, Gagiri amesema wakati wa mazungumzo hayo, Makuri hakukubaliana na ushauri aliokuwa akipewa na marehemu, hali iliyosababisha mvutano.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, Makuri alinyanyuka kutoka kwenye kikao na kwenda kuchukua panga, kisha akamfuata ndugu yake na kumkata shingo.

Baada ya tukio hilo, Gagiri amesema mtuhumiwa aliondoka katika eneo hilo usiku huo na kutokomea kusikojulikana.

Uchunguzi na hatua zaidi za kisheria zinatarajiwa kufuatia tukio hilo, huku taarifa rasmi kutoka Jeshi la Polisi kuhusu tukio hilo ikisubiriwa.

Related articles

Recent articles