Na Hassan Mwasha, Gazetini
MASHABIKI wa soka nchini bado hawajavutiwa na mwenendo wa timu yao ya Taifa ‘Taifa Stars’ tangu ilipoanza kunolewa na kocha wa kimataifa wa Argentina, Miguel Gamondi.
Tangu akabidhiwe mikoba ya kocha mzawa, Hemed Suleiman ‘Morocco’, Gamondi aliyewahi kuinoa Yanga kwa mafanikio, ameiongoza Stars katika michezo tisa ya mashindano na kirafiki.
Katika mechi hizo, Stars ya Gamondi imeshinda moja pekee [dhidi ya Macau inayoshika nafasi ya 193 kwenye viwango vya FIFA], imefungwa tano na kutoa sare tatu.
Kwa hivi karibuni, Stars imetoka kucheza dhidi ya Guinea Bissau na Madagascar, ambapo ilifungwa nyumbani [2-0] na kutoa sare ya ugenini [1-1].
Kwa mwenendo huo, wapo wanaoamini kocha huyo anastahili kupewa muda kwa kile alichowahi kukionesha akiwa na Yanga na Singida Black Stars, ingawa wengine wanaona hawezi kuipeleka Stars kwenye mafanikio.
Kwa wanaoamini Gamondi ni mtu sahihi, wana hoja kwamba katika mechi tisa alizokaa kwenye benchi, nne zilikuwa za AFCON 2025, zikiwamo dhidi ya vigogo Nigeria, Tunisia na Morocco.
Wakati huo huo, wanaojenga hoja yenye msingi wa kumkingia kifua kocha huyo wanaelekeza lawama kwa wachezaji, wakiamini hawajitoi
Hata hivyo, kwa wanaoona kocha huyo amechemsha, wanatolea mfano kupanda na kushuka kwa kiwango cha timu tangu Gamondi alipokabidhiwa mikoba.
Mathalan, licha ya kukosa ushindi, Stars ilicheza vizuri dhidi ya Nigeria, Tunisia na Morocco kwenye fainali za AFCON lakini haikuonesha kiwango hicho mbele ya Guinea Bissau na Madagascar, ambazo si timu za uzito wa juu barani Afrika.


