23 C
New York

Shilingi bilioni 198.67 kuimarisha umeme Songwe, Mbeya

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

SERIKALI imesaini mkataba wa Sh bilioni 198.67 kwa ajili ya ujenzi wa njia mpya ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 (220kV) kutoka Iganjo mkoani Mbeya hadi Saza mkoani Songwe, pamoja na ujenzi wa Kituo cha Kupokea na Kupoza Umeme cha Saza.

Mradi huo, unaotekelezwa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa kushirikiana na Kampuni ya TBEA, unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 18 na unalenga kuimarisha upatikanaji na uaminifu wa umeme katika maeneo ya Songwe na Mbeya, huku ukitoa msukumo kwa shughuli za kiuchumi ikiwamo uchimbaji wa madini.

Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, amesema mradi huo utasaidia kuongeza uwezo wa upatikanaji wa umeme na kupunguza changamoto zinazowakabili wananchi na shughuli za uzalishaji, hususan katika Wilaya za Chunya na Songwe.

Makamba ameyasema hayo Septemba 11, 2026, katika Kijiji cha Saza, Wilaya ya Songwe, wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa utekelezaji wa mradi huo.

Amesema kukamilika kwa mradi kutachochea uzalishaji katika sekta mbalimbali, ikiwamo kilimo cha kisasa, biashara na uchimbaji wa madini, huku kukiwa na matarajio ya kuboresha mazingira ya shughuli za kiuchumi katika maeneo yatakayohudumiwa na miundombinu hiyo.

“Napenda kuwahakikishia wananchi wa Songwe na Mbeya kwamba Serikali inaona changamoto za upatikanaji wa umeme katika maeneo yenu na inaendelea kuchukua hatua,” amesema Makamba.

Amesema ujenzi wa miundombinu hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali kujenga mfumo wa umeme wenye uwezo mkubwa zaidi wa kusafirisha na kusambaza nishati, sambamba na kuunganisha vizuri mifumo ya umeme.

Aidha, Makamba amesema ni muhimu wananchi kufahamu maendeleo ya Mradi wa TAZA (Tanzania–Zambia Transmission Interconnector Project), ambao ni sehemu ya mipango ya kuimarisha miundombinu ya usafirishaji wa umeme na kukuza biashara ya umeme katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Subira Mgalu, amepongeza Wizara ya Nishati na Tanesco kwa utekelezaji wa mradi huo, akisema utaleta manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi, ikiwamo fursa za ajira na kuchochea shughuli za uchimbaji wa madini.

“Mradi huu utakuwa na manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi, ikiwemo kuibua fursa za ajira na kuchochea shughuli za uchimbaji wa madini,” amesema Mgalu.

Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Tanesco, Balozi Zuhura Bundala, amesema shirika hilo linaendelea kuboresha miundombinu ya umeme ili kuendana na ongezeko la mahitaji ya nishati linalochochewa na shughuli za kiuchumi na kijamii.

Amesema mradi huo ni sehemu ya jukumu la Tanesco la kujenga miundombinu itakayokidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye, huku ikisisitiza matumizi yenye ufanisi ya fedha za mradi.

Naye Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco anayeshughulikia Mipango, Utafiti na Uwekezaji, Mha. Amos Joas, amesema changamoto iliyopo kwa sasa inatokana kwa kiasi kikubwa na mfumo wa usafirishaji wa umeme unaohudumia maeneo hayo.

Kwa mujibu wa Joas, maeneo ya Chunya na Songwe, hususan upande wa Mkwajuni, kwa sasa yanapata umeme kutoka Mkoa wa Mbeya kupitia Kituo cha Mwakibete kwa kutumia njia ya msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa zaidi ya kilomita 116.

Amesema umbali huo mrefu, sambamba na ongezeko la mahitaji ya umeme, umechangia changamoto katika upatikanaji wa umeme, hali ambayo mradi wa Iganjo–Saza unalenga kuiboresha.

Ujenzi wa njia ya 220kV kutoka Iganjo hadi Saza pamoja na Kituo cha Kupokea na Kupoza Umeme cha Saza unatarajiwa kuongeza uwezo wa miundombinu ya usafirishaji wa umeme na kuweka msingi wa kukidhi mahitaji yanayoongezeka katika maeneo hayo.

Mkataba wa utekelezaji wa mradi huo umesainiwa kati ya Serikali kupitia Tanesco na Kampuni ya TBEA, huku kazi zikitarajiwa kukamilika ndani ya miezi 18.

Related articles

Recent articles