TUNIS, Tunisia
“WALE wanaozikosoa mamlaka au mambo yanavyokwenda nchini Tunisia wanakumbana na ukandamizaji.” Ni kauli ya Messaoud Romdhani, mwanaharakati wa haki za binadamu katika nchi hiyo ya Afrika ya Kaskazini.
Romdhani anaongeza kuwa wakosoaji wa serikali wamejikuta wakibambikiwa kesi za utakatishaji fedha, lengo likiwa ni kuwazuia kufanya kazi yao.
Mwanaharakati mwingine ambaye hata hivyo hakutaka jina lake lifahamike katika mahojiano yake na DW, amesema hali hiyo imezua hofu na woga kwa wananchi kujadili hadharani baadhi ya mambo wasiyokubaliana nayo katika Serikali ya Rais Kais Saied.
Juni 25, 2026, yaliibuka maandamano makubwa nchini humo kupinga mwenendo wa Serikali iliyoko madarakani, wakiishinikiza kuwaachia huru wanaharakati na waandishi wa habari walioko gerezani.
Saied alichaguliwa katika uchaguzi mkuu wa kidemokrasia wa mwaka 2019 lakini miaka miwili baadaye alivunja bunge, kisha serikali yake kuodosha taasisi zingine za kidemokrasia, pamoja na kamatakamata ya viongozi wa upinzani.
Mbali na madai hayo, pia wananchi walieleza kutokuridhishwa na hali ya uchumi inayochagiza ugumu wa maisha, wakati huo huo wakilalamikia huduma mbaya za afya na uhaba wa ajira kwa vijana.
Agosti, 2026, wananchi walirudi barabarani wakishinikiza rais kujiuzulu. Katika moja ya jumbe zao, walisikika wakisema ‘Watu wanataka utawala ung’oke’.
Licha ya ukosolewaji huo, Saied amesisitiza mara kwa mara kwamba wanaomnyooshea kidole ni vibaraka wa mataifa ya nje na wamekuwa wakilipwa fedha kwa kazi hiyo.
Kwa upande wake, Shirika la Haki za Binadamu la Human Rights Watch, linatahadharisha juu ya hali mbaya ya uhuru wa kujieleza iliyopo Tunisia, ikieleza hilo kupitia ripoti yake ya hivi karibuni.
Katika hatua nyingine, bado kuna tofauti kubwa ya mitazamo kati ya vijana na wazee. Kundi la vijana, ambalo ni asilimia 30 ya raia wote, linaamini Serikali imefeli, wakati wakubwa zao [miaka 40 au zaidi] wanaona kuna mengi mazuri yamefanyika.


