PAYNESVILLE, Liberia
HIVI karibuni, Mahakama nchini Liberia ilimpa ruhusa ya kutoka gerezani Makamu wa Rais wa zamani, Jewel Howard-Taylor, ili kwenda kupata matibabu ya nje, kama walivyoomba wanasheria wake.
Hata hivyo, bado mashitaka dhidi yake yanaendelea na kutoka nje huko ni kwa masharti kadhaa, ikiwamo kukabidhi mahakamani nyaraka zake za kusafiria kwa hofu kwamba asije kutoroka.
Kabla ya hatua hiyo, siku chache zilizopita mamia ya raia wa Liberia walikusanyika nje ya Gereza la Monrovia wakati Rais wa zamani wa Taifa hilo, George Weah, alipokwenda kumtembelea baada ya taarifa za hali yake ya kiafya kuzorota.
Raia waliofika gerezani hapo kumsindikiza Weah ni wanachama na wafuasi wa Chama cha upinzani cha Congress for Democratic Change (CDC) wanaoipinga serikali ya Rais wa sasa, Joseph Nyuma Boakai.
Jewel, pamoja na raia wa kigeni watatu, wanashikiliwa na uchunguzi juu ya kuhusika kwao na mtandao wa usafirishaji wa dawa za kulevya, utakatishaji fedha, na uhalifu mwingine.
Bi. Jewel alikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Roberts, kisha kupelekwa makao makuu ya polisi, ikielezwa kuwa alikuwa kwenye harakati za kutorokea nje ya nchi.
Kwa wasiomfahamu, bi. Jewel aliyezaliwa mwaka 1963, aliwahi kuwa Seneta wa Jimbo la Bong kuanzia mwaka 2006 hadi alipoteuliwa kuwa Makamu wa Rais katika Serikali ya Weah mwaka 2018.
Aidha, huyo ndiye mke wa Rais wa zamani wa Liberia, Charles Taylor, ambaye kwa mujibu wa historia, aliingia madarakani mwaka 1997 baada ya kuongoza vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Baada ya kumng’oa madarakani aliyekuwa Rais wa Taifa hilo, Samuel Doe, Charles aliingia Ikulu lakini aliongoza kwa ‘mkono wa chuma’, akikandamiza wapinzani na kile aliyemkosoa.
Wakati huo huo, utawala wake ulisababisha vita kubwa kati ya Liberia na majirani zao, Sierra Leone, ambapo mamia ya raia walifariki na kujeruhiwa, achilia mbali waliokimbia makazi yao.
Hatimaye, Charles aliondoka madarakani mwaka 2003 na mwaka 2012 alihukumiwa kifungo cha miaka 50 gerezani kwa makosa ya uhalifu wa kivita. Anaitumikia hukumu hiyo huko Uingereza.


