MANCHESTER, Uingereza
GUMZO kubwa wakati wa usajili wa dirisha kubwa barani Ulaya uliofungwa Septemba 1, 2026, ni uhamisho wa kiungo Enzo Fernandez kwenda Manchester City akitokea Chelsea. Usajili wa pesa ndefu zaidi, Pauni milioni 125.
Nje ya uwanja, Enzo amekuwa kwenye mahusiano ya muda mrefu na mrembo aitwaye Valentina Cervantes. Wawili hao walikutana sekondari na tayari wana watoto wawili; Olivia na Benjamin.
Akisimulia safari ya uhusiano wao, Valentina anasema: “Nilikutana na Enzo wakati huo akiwa na umri wa miaka 16 na mwaka mmoja tu baadaye tulianza kuishi pamoja. Sote tunatokea San Martín na hata marafiki zetu ni wale wale.”
Mtoto wao wa kwanza, Olivia, alizaliwa mwaka 2020. Bibiye huyo anasema: “Olivia alipozaliwa, tulikuwa tunaishi kwenye nyumba yenye studio mjini Urquiza, ambapo wakala wa Enzo ndiye aliyekuwa akilipa (kodi).
“Wakati wa janga [Corona], sote watatu tulikuwa tunaishi hapo na nilikuwa nafanya kazi kwenye kituo cha miito ya simu, sikuwa hata nikilipwa mshahara. Tulimnunulia binti yetu nguo zilizotumika [mitumba] kupitia masoko ya Facebook. Wakati huo tulikuwa tunatumia usafiri wa umma …”
Mwaka 2022, Enzo aliondoka katika klabu ya River Plate na kujiunga na Benfica ya Ureno. Valentina na binti yake, Olivia, walihamia mjini Lisbon kuanza maisha mapya.
Hata hivyo, hawakudumu Ureno. Miezi mitano tu baadaye, Enzo alihamia Chelsea baada ya mabosi wa klabu hiyo kufika dau la Pauni milioni 107 lililovunja rekodi ya usajili katika historia ya soka la Uingereza.
Oktoba, 2023, Enzo na Valentina walitangaza kupata mtoto wao wa pili, safari hii akiwa ni wa kiume, Benjamin.
Lakini, licha ya kwamba wamedumu kwenye uhusiano, haimaanishi kuwa hawajawahi kuachana. Hiyo ilitokea kwa muda mfupi mwaka 2024, kabla ya kurudiana 2025.
Inaelezwa kuwa muda mfupi baada ya kuachana, Wanda Nara, mke wa zamani wa Mauro Icardi, alimtumia meseji za siri Enzo akimshawishi kutoka naye kimapenzi.
Kwa mujibu wa ripoti, haikuchukua muda mrefu, Enzo na Valentina walirudiana, ikisemekana kuwa jamaa aliamua kurejesha uhusiano baada ya kusikia kuna mchezaji mwenzake wa timu ya taifa ya Argentina anamtaka mrembo huyo.


