Na mwandishi wetu, Gazetini
WATU zaidi ya 80 walipoteza maisha kati ya Oktoba, 2025, hadi Julai, 2026, chanzo kikiwa ni uvumi wa taarifa za upotoshaji juu ya wizi wa sehemu za siri, kwa mujibu wa taarifa ya kiuchunguzi ya hivi karibuni ya Shirika la Utangazaji la Uingereza [BBC].
Kupitia Kitengo cha Habari za Upotoshaji, BBC ilikusanya taarifa zake kwa mahojiano na vyombo vya dola katika mataifa sita ya barani Afrika.
BBC imeeleza kuwa mauaji yalihusiana na kile kilichoelezwa kuwa watu waliotumia njia za kishirikina waliweza kuiba nyeti kwa kumgusa mtu kwenye bega.
Boniface Mgala, raia wa Tanzania na fundi magari aliyehojiwa na BBC, amesema akiwa na mwenzake walizingirwa na kisha kupigwa na kundi kubwa la watu waliodai kuwa wameiba nyeti za mtu mwingine.
“Walikuwa wakipaza sauti kwamba tumeiba nyeti za mtu, hatukuwa na namna ya kuepuka, maana kundi lilikuwa kubwa,” amesema Mgala.
Anachokizungumzia Mgala hakitofautiani na shuhuda nyingi za video zilizonaswa na BBC, ambapo wanaume kadhaa walidai kuwa nyeti zao zimepotea baada ya kuguswa bega na watu wasiowajua.
Hata hivyo, kwa mujibu wa BBC, taarifa hizo za uzushi juu ya wizi wa nyeti zilianza kuchomoza barani Afrika mwaka 2025, ambapo zilianzia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo [DRC].
Aidha, kwa mujibu wa Shirika hilo, madai kama hayo yaliwahi pia kusikika na kupata mwitikio makubwa katika jamii za DRC katika miezi fulani ya mwaka 2008.
Baadaye, madai hayo ya uzushi yalianza kuenea katika nchi jirani za Burundi, Zambia na Tanzania, kama ilivyo pia kwa Msumbiji, Angola, Malawi na Kenya.
Kwa upande wa Zambia, taarifa za aina hiyo zilianza Machi, 2026, baada ya mwanamke mmoja kueneza kuwa ameibiwa sehemu zake za siri. BBC inadai kuwa taarifa hizo zilivuka mpaka na kuingia Tanzania.
Katika mahojiano yake na BBC, Mgala ambaye ni mkazi wa Mpemba, eneo lililoko jirani na Tunduma, ambako ni mpakani mwa Tanzania na Zambia, anasema siku ya tukio alikuwa na rafiki yake wakipata chakula katika mgahawa fulani.
Kwa mujibu wake, walifika hapo Aprili 1, 2026, kwa ajili ya kumsubiri mteja wa gari. “Muda mfupi baadaye, lilikuja kundi la watu na kututoa nje, kisha kuanza kutupiga,” amesema.
Anaongeza kuwa kichapo hicho cha raia kilisababishia apoteze fahamu na kuzinduka siku mbili baadaye akiwa hospitali. Rafiki yake alipoteza maisha siku ya tukio.
Si tu kupoteza meno yote, pia Mgala, baba wa watoto wanne, anakiri kuwa amekuwa akisumbuliwa na maumivu ya kichwa tangu ‘alipochungulia kaburi’ katika kichapo hicho.
Katika stori nyingine, mpigajipicha ambaye pia ni mfanyabiashara, Michael Silavwe, anasema aliwahi kushuhudia tukio jingine la aina hiyo hapo Tunduma.
Kwa mujibu wake katika mahojiano yake na BBC, Silavwe anasema nje ya ofisi yake alikamatwa mwanaume na baada ya kupigwa kwa madai ya kuiba nyeti, aliuawa kwa kuchomwa moto.
“Baada ya kumchoma moto, polisi walifika na hapo kila mtu alikimbia,” amesema Silavwe mwenye umri wa miaka 23 kuiambia BBC.
Katika video nyingine iliyonaswa na BBC ikiwa imetazamwa mara zaidi ya 100,000 katika mitandao miwili ya TikTok na Facebook, kundi la watu linaonekana likimpiga mwanaume mmoja huku likimshinikiza kurehesha nyeti alizoiba.
BBC iliweza kupata video za aina hiyo katika nchi zingine za Msumbiji na Kenya. Kwa Msumbiji, hofu ilitawala zaidi katika Mkoa wa Kaskazini wa Cabo Delgado, ambako idadi ya watu ni ndoto kutokana na vita.
Hata hivyo, Asha Steven Mwakilasa, mjasiriamali wa ushonaji wa nguo wilayani Momba, Tunduma, anasema licha ya hofu iliyojengeka wakati huo, alikuja kubaini kuwa hazikuwa taarifa za kweli.
Mwisho, Mgala naye anaunga na Asha, akisema inamuumiza hadi sasa kuona uzushi ulisababisha kifo cha rafiki yake.
NB: Makala haya yaliandikwa kwa lugha ya Kiingereza katika tovuti ya BBC, kisha GAZETINI kuitafsiri kwa Kiswahili ili kukidhi mahitaji ya hadhira yake.


