TRIPOLI, Libya
BAADA ya mvutano wa muda mrefu kati ya kati ya serikali mbili, walau wananchi wa Libya wameanza kuona mwanga wa kurejea kwa amani baada ya pande hizo kukubaliana kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu.
Kwa msaada wa Umoja wa Mataifa [UN], Serikali iliyoko Magharibi na ile ya Mashariki, kwa pamoja zimekubali Uchaguzi ufanyike ndani ya miaka miwili ijayo.
Mbali na mambo mengine, pande mbili hizo zimefikia makubaliano pia ya kuifumua tume ya sasa ya uchaguzi, kwa mujibu wa UN.
Tangu mwaka 2014, miaka mitatu baada ya kiongozi wake, Moammar Gadhafi, alipouawa, Libya imekuwa kwenye mpasuko uliozaa serikali mbili ndani ya nchi hiyo.
Serikali moj imekuwa ikishikilia na kuongoza maeneo ya Mashariki na nyingine mamlaka yake yako upande wa Magharibi.
Aidha, ile ya Magharibi ndiyo inayoungwa mkono na UN na iko katika Mji wa Tripoli, wakati wapinzani wao, ambayo imekuwa ikijiita Bunge, iko Mashariki katika Mji wa Tobruk.
Kiongozi wa zamani wa waasi aliyegeuka mwanasiasa, Khalifa Haftar, yuko Mashariki, wakati ile ya Magharibi inaye Waziri Mkuu, Abdul-Hamid Dbeibah.
Kila mmoja kwa upande wake anaungwa mkono na vikundi vya kijeshi vya ndani na jumuhiya za kimataifa, lengo likiwa ni kuongeza ushawishi na mamlaka ndani ya Libya.
Aidha, mvutano na hata mapigano ya pande mbili hizo wakati fulani yamezalisha hali mbaya ya kiusalama katika maeneo mengi.
Hata hivyo, makubaliano ya safari ya kutafuta suluhu bado hayatoi picha ya moja kwa moja, kwamba Libya inakwenda kurejesha utulivu wa kisiasa. Kwanini?
Hii si mara ya kwanza kuwapo kwa jitihada za upatanishi lakini zote hazikuweza kuzaa matunda. Marekani kupitia kwa Mshauri wa Rais Donald Trump katika masuala ya nchi za Kiarabu na Mashariki ya Kati, Massad Boulos, imejaribu bila mafanikio.
Kama hiyo haitoshi, Juni, 2026, mtoto wa kiume wa Haftar, Saddam, alikuwa mjini Washington, Marekani, na kukutana na Katibu Mkuu wa Serikali, Marco Rubio.
Wakati huo huo, wapo wanaohoji, serikali mpya itakayochaguliwa itaweza kujiepusha na ushawishi wa pande mbili hizo?
Mwisho, wananchi wa Libya wanataka amani, pia utajiri wa mafuta walionao ukiondosha changamoto lukuki zinazowakabili, ikiwamo umeme usio wa uhakika na mdororo wa huduma za kijamii.


