RABAT, Morocco
KUELEKEA Uchaguzi wa Wabunge wa Septemba 23, 2026, wanasiasa nchini Morocco wataanza mikutano ya kampeni ifikapo Septemba 10.
Wagombea zaidi ya 700 kutoka vyama vya siasa 27 wamechukua fomu, kwa mujibu wa kile kilichoelezwa na Wizara ya Mambo ya Ndani nchini humo.
Wananchi takribani milioni 15.8 wamejiandikisha kupiga kura, sawa na asilimia 36.8 ya raia wote wa nchi hiyo, kwa mujibu wa Sensa ya Mwaka 2024.
Katiba ya Morocco inaeleza kuwa wananchi watapiga kura, kisha chama kitakachoongoza kwa idadi ya wabunge ndicho kitakachoongoza mchakato wa kuunda serikali.
Baada ya hapo, Katiba inamtaka Mfalme wa nchi hiyo kuteua kiongozi wa Serikali kutoka katika chama kilichoongoza kwa idadi ya wabunge.
Hata hivyo, kwa Morocco, chama kuwa na wabunge wengi hakumaanishi nguvu ya moja kwa moja, bali bado kitapaswa kushirikiana na vyama vingine katika uendeshaji wa serikali.
Mathalan, serikali ya sasa inaongozwa kwa ushirikiano wa vyama vitatu; National Rally of Independents [RNI], Authenticity and Modernity Party [PAM] na Istiqlal.
Kwa sasa, kila kimoja kimeingia kwenye vita ya kusaka kura na ushawishi wa wananchi ili kiweze kuvuna kura nyingi katika Uchaguzi ujao.
RNI kilichoongoza kwa wabunge wengi katika Uchaguzi uliopita wa mwaka 2021 baada ya kukusanya kura 102, kwa sasa kinapambana kutetea nafasi yake bungeni.
Katika Uchaguzi huo, PAM kilipata kura 87, wakati Istiqlal kiliambulia 81. Licha ya RNI kuviacha mbali, bado vyama vitatu hivyo viliunda serikali ya pamoja.
Kwa upande mwingine, Chama kikongwe, Justice and Development (PJD) nacho kinapewa nafasi kubwa katika Uchaguzi wa mwaka huu.
PJD kiliunda serikali kwa mihula miwili, kuanzia mwaka 2011 hadi 2021, kabla ya kuangushwa kikiwa na kura 13 pekee.
Mara zote wanasiasa wake wamekuwa wakiishutumu serikali ya sasa katika maeneo ya kupanda kwa bei ya bidhaa, uhaba wa ajira, na kudorora kwa huduma za kijamii, zikiwamo sekta za afya na elimu.


