Na mwandishi wetu, Gazetini
SIKU chache zilizopita, Mahakama mjini The Hague, Uholanzi, ilimuhukumu kifungo cha maisha mwanaume aliyetambulika kwa jina la Eugene N baada ya kukutwa na hatia ya kushiriki mauaji ya halaiki dhidi ya Watutsi katika vita vya mwaka 1994 nchini Rwanda.
Historia inakumbusha kuwa katika vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe nchini Rwanda vya mwaka 1994, Watutsi zaidi ya 800,000 waliuawa na Wahutu.
Vita hivyo vya siku 100, kuanzia Aprili-Julai, 1994, vilishuhudia Wahutu takribani 200,000 wakihusika katika mauaji dhidi ya Watutsi. Kutokana na machafuko, raia wa Rwanda 2,000,000 waliikimbia nchi yao.
Eugene, raia wa Uholanzi aliyezaliwa Rwanda, alitajwa na mahakama kuongoza kikundi cha jamii ya Wahutu kuvamia nyumba za Watutsi, kisha kuwapiga, kujeruhi na kuua.
Pia, katika moja ya matukio ya kikatili, alishirikiana na wenzake kurusha bomu kwenye mkusanyiko watu wa jamii hiyo waliokuwa uwanjani wakitazama mechi ya soka.
Kwa upande wake, Eugene ametajwa na mahakama kuhusika moja kwa moja katika matukio yaliyosababisha vifo vya Watutsi 3,000 mjini Mbazi, Kusini mwa Rwanda.
“Kwa uhalifu wa mshitakiwa, ambapo alichangia vifo vya watu wasio na hatia takribani 3,000, ikiwamo kurusha bomu kwenye uwanja wa soka, nini kingine anachostahili kama si kifungo cha maisha gerezani?” alihoji mmoja ya waendesha mashitaka.
Hata hivyo, Eugene alijitetea akisema hajahusika kwa namna yoyote ile kwenye matukio yanayotajwa. Alisisitiza kuwa yeye pia ni muhanga wa vita kwani alipoteza makumi ya ndugu zake.
Akithibitisha utetezi huo, mmoja ya wanasheria wake alisema Eugene alifanya kila linalowezekana kuzuia mauaji wakati wa vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe. “Kesi hii imetonesha kidonda chake. Ameumizwa,” alisema mwanasheria wake.
Itakumbukwa kuwa Eugene alikimbilia Uholanzi mwaka 1998 na tangu kipindi hicho amekuwa raia wa nchi hiyo. Kutokana na uraia wake, Uholanzi ilishindwa kumkabidhi kwa Serikali ya Rwanda, licha ya waendesha mashitaka wa nchi hiyo ya Afrika kuomba akamatwe mwaka 2014.
Na badala yake, waendesha mashitaka wa Uholanzi waliamua kuanzisha uchunguzi binafsi dhidi yake mwaka 2020. Ni baada ya mashahidi kadhaa kutoka Rwanda kuhojiwa, Eugene alikamatwa mwaka 2024.
Nini chanzo cha mauaji ya halaiki nchini Rwanda? Tukutane katika sehemu ya pili ya makala haya. Tembelea www.gazetini.co.tz.


