19.8 C
New York

Kesi ya uhaini inavyowatesa wanasiasa wa upinzani Afrika

Published:

LUSAKA, Zambia

KIONGOZI wa siasa za upinzani nchini Zambia, Brian Mundubile, na mgombea mwenzake wake katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika hivi karibuni, Makebi Zulu, wameshikiliwa na polisi na kuhojiwa kwa tuhuma za uhaini.

Mundubile, mwanasheria mwenye umri wa miaka 55, aligomea matokeo baada ya Tume ya Uchaguzi kumtangaza mpinzani wake, Hakainde Hichilema, kushinda kiti cha urais kwa asilimia 60 ya kura.

Aidha, Mundubile aliyepata asilimia 38 ya kura, alilazimika kujikabidhi mikononi mwa polisi baada ya wiki mbili za kujificha kwa kile alichokiita jumbe za kutishiwa maisha.

Hata hivyo, Mundubile si mwanasiasa wa upinzani wa kwanza barani Afrika kuangukiwa na kesi ya uhaini (kitendo cha kuisaliti nchi kwa kusaidia maadui au kujaribu kuiondoa serikali halali iliyoko madarakani). Hawa ni baadhi yao tu.

KIZZA BESIGYE (UGANDA)

Kiongozi wa Chama cha Forum for Democratic Change (FDC). Serikali ya Rais Yoweri Museveni ilimfungulia kesi ya uhai mwaka 2015, kabla ya Mahakama kumkuta hana hatia baada ya kukosekana kwa ushahidi juu ya shutuma hizo.

Mwaka 2024, Besigye alikamatwa na kufunguliwa tena mashitaka ya uhaini. Bado anakabiliwa na kesi hiyo, licha ya kwamba hali yake ya kiafya imeripotiwa kuwa mbaya.

MOISE KATUMBI (DRC)

Gavana wa zamani wa Jimbo la Katanga. Akiwa mshindani mkubwa wa Joseph Kabila katika kinyang’anyro cha urais, Katumbi alikamatwa na kushitakiwa kwa kosa la uhaini mwaka 2016.

Katumbi alikimbilia uhamishoni nchini Ubelgiji, kabla ya kurejea mwaka 2019 na maisha yakaanza upya bila kesi chini ya utawala mpya wa Rais Felix Tshisekedi.

JULIUS MALEMA (AFRIKA KUSINI)

Ni kada wa zamani wa Chama kikongwe cha African National Congress (ANC), na sasa Malema amebeba sura ya upinzani katika siasa za Afrika Kusini akiwa kiongozi wa Chama cha Economic Freedom Fighters (EFF).

Mwaka 2016, ANC ilimfungulia mashitaka ya uhaini baada ya mahojiano yake aliyofanya na kituo cha televisheni cha Al Jazeera. Alisema Chama chake kingetumia hata vurugu kukabilia na Serikali ya ANC. Kesi ilipotea baada ya uchuguzi wa polisi.

MORGAN TSVANGIRAI (ZIMBABWE)

Kiongozi wa Chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change (MDC) aliyekuwa akishindana vikali na Hayati Robert Mugabe katika kinyang’anyiro cha urais.

Mwaka 2003, Tsvangirai alifunguliwa kesi ya uhai akidaiwa kusuka mpango wa kumuua Mugabe kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2002. Kesi hiyo ilimwendesha Tsvangirai kwa mwaka mmoja, kabla ya Mahakama Kuu ya Harare kumkuta hana hatia.

VICTOIRE INGABIRE UMUHOZA (RWANDA)

Wakati fulani, bi. Victorie aliwahi kuwa mpinzani mkubwa wa Rais Paul Kagame katika siasa za Rwanda. Mwaka 2012, alihukumiwa miaka nane gerezani kwa kosa la uhaini, kisha adhabu ikaongezeka na kufikia miaka 15.

Hata hivyo, alipata msamaha wa rais mwaka 2018, kabla ya kukamatwa tena Juni, 2025 kwa makosa mbalimbali, ikiwamo kuunda kikundi cha uhalifu. Wanaharakati, zikiwamo jumuhiya za kimataifa, wanaona kesi dhidi yake ni siasa chafu cha utawala wa Rais Kagame.

Related articles

Recent articles