Na mwandishi wetu, Gazetini
KENYA imetangaza kuondosha kigezo cha kuwa na Shahada ya chuo kikuu kama kigezo cha mgombea wa kiti cha urais. Hii ni pamoja pia na wagombea wa Ugavana na Ubunge kuanzia Uchaguzi Mkuu ujao (2027).
Mabadiliko hayo yanaifanya Kenya sasa kuwa kama baadhi ya nchi za Afrika, zikiwamo Nigeria, Ghana, Afrika Kusini na Uganda, ambazo mgombea wa nafasi hizo halazimiki kuwa na ‘digrii’.
Aidha, mabadiliko hayo ya Kenya yanafungua milango kwa wananchi wengi zaidi kugombea urais, ikizingatiwa kuwa wenye digrii ni asilimia 3.5 tu ya raia wote wa nchi hiyo.
Kwa upande wa Nigeria, inatosha tu kwa mgombea wa nafasi ya urais kuwa na elimu ya sekondari, pia vikiwepo vigezo vya uraia wa kuzaliwa, umri na kufadhiliwa na chama cha siasa.
Uganda, kwa upande wake, ili kugombea urais, lazima uwe mbunge na ili kuingia bungeni, lazima uwe na walau elimu ya sekondari ya juu (A-Level).
Aida, ili kugombea urais nchini Ghana, vigezo ni uraia wa kuzaliwa, umri wa walau miaka 40 na sifa za kuwa mbunge, bila kujalisha kiwango cha digrii kwa upande wa elimu.
Ni kama ilivyo kwa Afrika Kusini, ambako pia elimu ya kiwango cha digrii siyo ishu kwa mgombea wa nafasi ya urais.


