19.8 C
New York

Kivuli cha Lungu kinamfuata Rais Hichilema?

Published:

LUSAKA, Zambia

LICHA ya kutangazwa mshindi katika Uchaguzi Mkuu wa hivi karibuni, Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema, anakabiliwa na presha kubwa ya ‘kumtuliza’ mpinzani wake, Brian Muntayalwa Mundubile.

Mundubile hajakubali matokeo ya Tume yaliyompa Hichilema ushindi wa asilimia 60 ya kura, huku yeye akiambulia asilimia 38. Anahisi kuna namna amechezewa faulo.

Matokeo ya hayo si tu yamepingwa ndani, bali hata jumuhiya za kimataifa zimedai kuwa Uchaguzi haukuwa huru na wa haki, hasa kwa vyama vya upinzani.

Katika kile kilichotafsiriwa kuwa ni kumtuliza na kurejesha utulivu unaoonekana kutokuwa kwenye kiwango chake, mamlaka zinamshikilia Mundubile, ikielezwa kuwa anakabiliwa na kesi ya uhaini.

Je, ni nani huyo Mundubile? Makala haya yanatazamia mengi usiyoyajua kuhusu kiongozi huyo wa Chama cha Patriotic Front (PF), ambaye kitaaluma ni muhasibu na mwanasheria. Endelea nayo.

Alizaliwa Januari 5, 1971, huko Mporokoso, Kaskazini mwa Zambia. Safari yake katika siasa ilianzia katika Chama hicho cha PF na aliingia Bungeni mwaka 2016 akiwakilisha Jimbo la Mporokoso, kabla ya kutetea kiti chake katika Uchaguzi uliofuata (2021).

Katika hatua hizo za awali, PF kilikuwa chini ya Edgar Lungu, ambaye wakati huo alikuwa Rais wa Zambia. Baadaye, Mundubile alihudumu katika nafasi mbalimbali za serikali ya Lungu.

Wakati ambao Lungu aliweza kumfunga gerezani Hichilema, ambaye wakati huo alikuwa mshindani wake mkubwa katika kiti cha urais kupitia United Party for National Development (UPND).

Hata baada ya Hichilema kumbwaga Lungu katika Uchaguzi Mkuu wa 2021, naye hakuacha yaishe. Lungu alisota gerezani kwa kesi zilizotafsiriwa na wengi kama kisasi.

Wakati huo, Mundubile akawa kiongozi wa upinzani bungeni kupitia PF, akichukua nafasi ya bosi wake, Lungu, kabla ya kupoteza nafasi hiyo mwaka 2023 baada ya mabadiliko makubwa yaliyofanyika ndani ya Chama.

Lungu alipofariki mwaka 2025, Mundubile akalazimika kuvaa viatu vyake kumkabili Hichilema katika Uchaguzi huu wa mwaka 2026. Safari hii, haikuwa PF pekee, bali muunganiko wa vyama vya upinzani uliopewa jina la Tonse Alliance.

Katika kampeni zake, Mundubile aliwakumbusha mara zote wananchi wa Zambia juu ya kupanda kwa gharama za maisha, umasikini, kuporomoka kwa sekta ya kilimo, uhaba wa ajira, na uminywaji wa demokrasia.

Related articles

Recent articles