Na Faraja Mulungu Gazetini
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) si “white elephant”, bali ni mradi wa kimkakati wenye manufaa makubwa kwa Taifa, ikiwemo kuongeza upatikanaji wa umeme, kuchochea uwekezaji na kukuza shughuli za kiuchumi.
Rais Samia ameyasema hayo leo, Jumamosi, Agosti 22, 2026, wakati wa uzinduzi rasmi wa mradi huo wilayani Rufiji mkoani Pwani, akieleza kuwa mradi huo tayari umeanza kuonesha manufaa kwa kuongeza uwezo wa Taifa kuzalisha umeme.
“Mradi huu siyo white elephant. Una manufaa makubwa kwa Taifa letu na utaendelea kuwa na manufaa kwa muda mrefu,” amesema Dk. Samia.
Amesema kituo hicho kinachangia sehemu kubwa ya umeme unaotumika nchini, hatua ambayo imeongeza uwezo wa Taifa kuwa na umeme wa uhakika na akiba kwa ajili ya shughuli mbalimbali za uzalishaji.
“Leo tunaona manufaa yake. Uzalishaji wa umeme umeongezeka na tuna uwezo wa kuwa na umeme wa kutosha kwa ajili ya viwanda, biashara na shughuli nyingine za kiuchumi,” amesema.
Kwa mujibu wa Rais Samia, upatikanaji wa umeme wa uhakika ni kichocheo cha maendeleo kwa kuwa unawawezesha wawekezaji kuanzisha na kupanua shughuli zao, huku ukitoa fursa zaidi za ajira na kuongeza uzalishaji.
Amesema Serikali inaendelea na ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha umeme unaozalishwa katika mradi huo kwenda maeneo mbalimbali nchini.
“Hatujajenga kituo hiki peke yake, tunaendelea pia kujenga njia za kusafirisha umeme ili kuhakikisha umeme huu unawafikia Watanzania na kuchochea maendeleo ya Taifa,” amesema.
Rais Samia pia amesisitiza umuhimu wa kulinda mazingira na vyanzo vya maji vinavyolisha bwawa la JNHPP, akisema uendelevu wa mradi huo unategemea kwa kiasi kikubwa uhifadhi wa mazingira na vyanzo hivyo.
“Tukiharibu mazingira na vyanzo vya maji, tutakuwa tunaiweka rehani miradi yetu wenyewe. Ni lazima tushirikiane kuhakikisha vyanzo hivi vinalindwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo,” amesema.
Amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika vyanzo mbalimbali vya nishati, ikiwemo maji, jua na upepo, ili kukidhi ongezeko la mahitaji ya umeme.
Waziri Ndejembi
Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amesema Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu ya kusafirisha umeme ili kuhakikisha ongezeko la uzalishaji kutoka JNHPP linafika kwa uhakika katika maeneo mbalimbali nchini.
Amesisitiza kuwa kuongeza uwezo wa kuzalisha umeme pekee hakutoshi bila kuwepo kwa mtandao imara wa kupokea na kusafirisha nishati hiyo.
“Kuongeza uzalishaji wa umeme pekee haitoshi bila kuwa na miundombinu imara ya kusafirisha umeme huo kwenda kwa watumiaji,” amesema Ndejembi.
Amesema njia ya kusafirisha umeme ya kV 400 Chalinze-Dodoma imekamilika na kuongeza uwezo wa kusafirisha umeme, huku kiwango cha juu cha matumizi ya umeme nchini kikiongezeka kutoka MW 2,130 hadi MW 2,280 ndani ya siku tatu.
Serikali pia inaendelea na miradi ya Chalinze-Mkuranga-Kinyerezi, Iringa-Mbeya-Tunduma/Sumbawanga, Songea-Tunduru-Masasi-Mahumbika pamoja na upanuzi wa Kituo cha Ibadakuli, Shinyanga.
Ndejembi amesema kwa sasa Tanzania ina uwezo wa kuzalisha takribani MW 4,646, huku Serikali ikilenga kufikisha MW 8,000 ifikapo mwaka 2030 kupitia vyanzo mbalimbali vya nishati.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Lazaro Jacob Twange, amesema ujenzi wa Bwawa la Kuzalisha Umeme la Mwalimu Nyerere umewezesha Watanzania kupata ujuzi na uzoefu mkubwa katika utekelezaji wa miradi mikubwa.
Twange amesema zaidi ya asilimia 95 ya waliofanya kazi katika ujenzi wa mradi huo walikuwa Watanzania, hivyo uzoefu walioupata utawasaidia kushindana katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.
Amesema mhandisi mshauri wa mradi huo pia alikuwa Mtanzania, jambo alilosema limejenga uwezo kwa wataalamu wa ndani na kuthibitisha kuwa Watanzania wanaweza kusimamia miradi mikubwa.
“Mhandisi mshauri pia alikuwa Mtanzania… imeonesha kuwa Watanzania tunao uwezo wa kusimamia miradi mikubwa na ikamalizika kwa wakati,” amesema.
Twange amesema kituo hicho ni mhimili wa usalama wa Taifa na ameahidi Tanesco kuboresha mifumo ya udhibiti na matengenezo ya mitambo, huku ikishirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha ulinzi madhubuti.
Aidha, amesema uendelevu wa uzalishaji umeme katika bwawa hilo unategemea upatikanaji wa maji, hivyo Tanesco itaendelea kushirikiana na wadau wa mazingira katika kulinda vyanzo vya maji vinavyolisha bwawa hilo.
Mbowe ashiriki
Katika uzinduzi wa mradi huo kiongozi wa zamani wa Chadema, Freeman Mbowe, alikuwa ni sehemu ya watu walioshiriki ambapo uwepo wake ulikuwa ni katibya mambo yaliyopamba hafla hiyo iliyodumu kwa saa tatu
Mbowe, ambaye ni mmoja wa viongozi wa upinzani waliowahi kutoa mitazamo mbalimbali kuhusu miradi mikubwa ya taifa, alishuhudia tukio hilo lililobeba ujumbe wa mshikamano katika kutambua mchango wa Watanzania mbalimbali katika ujenzi wa mradi huo.
Mawaziri wanne wa zamani wa Nishati ambao ni Profesa Sospeter Muhongo, Merdad Kalemani, January Makamba na Dotto Biteko walitambuliwa kwa mchango wao katika hatua mbalimbali za utekelezaji wa JNHPP.
Rais Samia amewatunuku mawaziri hao tuzo maalum kama ishara ya kutambua mchango wao katika kusukuma mbele mradi huo wa kimkakati.
Tuzo hizo ziliibua taswira ya kwamba miradi mikubwa ya kitaifa si matokeo ya kipindi kimoja cha uongozi, bali hujengwa hatua kwa hatua na viongozi na wataalamu mbalimbali.
Kwa waliohudhuria, tukio hilo lilikuwa zaidi ya uzinduzi wa mradi; lilikuwa pia jukwaa la kutambua historia, juhudi na watu waliowahi kushiriki katika safari ya kuhakikisha Tanzania inakuwa na uhakika wa nishati kwa maendeleo ya taifa wakiwamo mwasisi wa mpango huo Hayati, Julias Nyerere, hayati Ali Hassan Mwinyi, hayati Benjamini Mkapa, Jakaya Kikwete na hayati Dk. Jonh Magufuli.


