Na mwandishi wetu, Gazetini
VURUGU na chuki dhidi ya wageni zina uhusiano wa moja kwa moja na maisha magumu walionao wananchi wa Afrika Kusini katika maisha yao ya kila siku huko mitaani.
Vijana walio wengi wamepoteza matumaini kutokana na uhaba wa ajira, huku Chama tawala, African National Congress (ANC), kikiwa hakina namna ya kuepuka lawama.
Mchambuzi wa siasa kutoka Taasisi ya Rosa Luxemburg, Fredson Guilengue, chuki dhidi ya wageni ni ujumbe wa Waafrika Kusini kwamba wamechoshwa na mkwamo wa Chama kikongwe hicho katika kutatua changamoto zao.
“Inaakisi kuchoshwa na namna ANC ilivyoshindwa kitaifa na katika ngazi za chini kutengeneza ajira, kuondosha ukosefu wa usawa, kupunguza uhalifu, na kuboresha hali ya maisha,” amesema Guilengue.
Kuelekea Uchaguzi mdogo wa Novemba, 2026, wengi wanaona ANC itakabaliwa na maswali magumu juu ya ajira, hali mbaya ya huduma za afya, miundombinu isiyojisholeza, na umasikini.
“Changamoto hizo hazijafanyiwa kazi kwa miaka mingi na sasa zimeota mizizi katika jamii. Halimashahuri ziko chini ya ANC lakini miundombinu iko kwenye hali mbaya,” amesema.
Eneo jingine lililoonekana kuwa tatizo kubwa kwa ANC ni namna Chama hicho kilivyofeli katika kudhibiti vitendo vya rushwa serikalini.
Mbaya zaidi, Rais Ramaphosa, ambaye hatogombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2029, alikwaa kashfa nzito ya kuficha mamilioni ya Dola za Marekani kwenye sofa.
Kuelekea Uchaguzi mdogo wa Novemba 4, 2026, ANC ina kumbukumbu ya kufanya vibaya katika Uchaguzi Mkuu uliopita (2024), ambapo Rais Cyril Ramaphosa alishinda muhula wake wa pili kwa asilimia 40.2 tu ya kura.
Ushindani mkali ulitoka kwa Chama Kikuu cha upinzani, Democratic Alliance (DA), ambacho kilipata nafasi ya kuunda Serikali ya Umoja.
Kwa wachambuzi walio wengi, huenda safari hii katika Uchaguzi wa Novemba, wapiga kura wakakigeukia DA, ambacho kwa kiasi kikubwa kinaungwa mkono na Waafrika Kusini weupe.
Wakati huo huo, kipo Chama cha MK, kikifahamika pia kwa jina la uMkhonto weSizwe, ambacho kinaongozwa na Rais wa zamani, Jacob Zuma.
Vilevile, vyama vingine vya upinzani ni pamoja na (Patriotic Alliance), Freedom Front Plus na ActionSA.


