30 C
New York

Vichocheo vya kufikia malengo ya Dira 2050: Utafiti na Maendeleo

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

KADRI nchi inavyoendelea, utfiti na maendeleo ni nyenzo muhimu katika kuongeza ubunifu, kutatua changamoto za ndani, na kuongeza tija katika uzalishaji.

Vilevile, utafiti na maendeleo huimarisha ukuzaji wa ustadi, husaidia kutoa mwongozo wa uundaji wa sera, na kukuza mbinu endelevu za maendeleo, hivyo kuimarisha ushindani wa nchi kwenye soko la kimataifa.

HATUA ZILIZOPIGWA

Kwa kutambua umuhimu huo, Serikali imechukua hatua madhubuti za kuongeza kasi ya utafiti, ikiwa ni pamoja na kuongeza bajeti ya utafiti, kuimarisha ushirikiano baina ya vyuo vikuu, taasisi za utafiti na sekta za uzalishaji na huduma.

Mbali ya hatua hizo zenye tija kubwa, pia Serikali imeongeza juhudi za kuhamasisha maendeleo na matumizi ya teknolojia bunifu.

Hatua hizo zimechochea ongezeko la kiwango cha ubunifu, ambalo linadhihirishwa na kuongezeka kwa kampuni zinazochipukia, vituo vya ubunifu, vituo vya kulea na kustawisha mawazo ya biashara na programu za ukuaji wa biashara.

Aidha, taasisi za elimu nchini zimeongeza mkazo kwenye utafiti na maendeleo, sambamba na kuimarisha mifumo ya kulinda hakimiliki, jambo linalosaidia kuhifadhi haki za wabunifu na kukuza utamaduni wa ubunifu na uvumbuzi.

CHANGAMOTO ZILIZOPO

Hata hivyo, eneo hilo la utafiti na maendeleo linakabiliwa na changamoto kadhaa, zikiwamo za uhaba wa fedha, miundombinu isiyotosheleza na ushirikiano mdogo baina ya wadau.

Mbali ya hayo, pia kuna changamoto za sheria, upungufu wa wataalamu kutokana na kuhama kwa nguvukazi, uelewa mdogo wa umma, na tofauti za kijinsia zinazoendelea kukwamisha shughuli za utafiti na maendeleo.

MATARAJIO

Mosi, ni kuwa na mfumo imara wa utafiti na maendeleo unaovutia ushirikiano wa kimataifa, ukiimarishwa na ulinzi Madhubuti wa hakimiliki ili kuchochea ubunifu na kuendeleza uwekezaji.

Pili, kuwa na mfumo wa uhakika wa kugharamia utafiti na maendeleo, kwa kutumia kiwango kisichopungua asilimia moja ya Pato la Taifa, na unaotoa motisha kwa sekta binafsi kuwekeza kuwekeza katika sekta muhimu kama kilimo, bioteknolojia, nishati safi na teknolojia zinazoibukia katika TEHAMA na nyanja zingine.

Tatu, kuwa na Taifa lenye mtazamo wa kimaendeleo na utamaduni wa kufanya maamuzi kwa kutegemea ushahidi wa kisayansi, likichochewa na utatifi wa kiwango cha juu ili kumarisha maendeleo ya jamii na kiuchumi.

Nne, Tanzania kuwa kitovu cha ubunifu cha kikanda kinachochochea uvumbuzi kwa wataalamu wa ndani na kinachotoa huduma kamili za ubunifu, kuanzia uvumbuzi hadi kufanya biashara.

Tano, kuwa na vyuo vya elimu ya juu na taasisi mahiri za utafiti zenye viwango vya kimataifa, na zenye ushirikiano thabiti na sekta mbalimbali kwa ajili ya kuchochea ubunifu kwenye uzalishaji na kutatua changamoto za kijamii.

Sita, kuwa na mfumo imara wa kuendeleza ubunifu unaoendana na maendeleo ya kiteknolojia, na utakaoifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa uvumbuzi duniani.

Related articles

Recent articles