30.9 C
New York

Simba hoi, Yanga ‘yapiga kwenye mshono’ ikibeba Ngao ya Jamii

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini 

WAKATI maumivu ya kupokonywa Selemani Mwalimu yakiwa hayajapoa, Yanga imeipiga tena Simba kwenye mshono kwa kuifunga bao 1-0 na kutwaa taji la Ngao ya Jamii katika ‘derby’ iliyochezwa katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Katika mechi hiyo ya leo Agosti 12, 2026, Yanga ilipata bao hilo kupitia kwa nyota wake mpya raia wa Zambia, Albert Kangwanda.

Kangwanda, mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Zambia msimu uliopita (2025-26), alijiunga na ‘Timu ya Wananchi’ hivi karibuni akitokea Red Arrows FC.

Dhidi ya Simba, alifunga bao hilo katika dakika ya 31, akiunganisha kwa kichwa krosi ya beki wa kushoto raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Chadrack Issaka Boka.

Kwa ushindi huo, Yanga imefikisha mataji 10 ya Ngao ya Jamii, sawa na Wekundu wa Msimbazi, ambao pia wana idadi hiyo.

Kabla ya kubeba tena leo, Wanajangwani hao walitwaa mataji hayo mwaka 2001, 2010, 2013, 2014, 2015, 2021, 2022, 2024, na 2025.

Kwa upande wao, Simba walikuwa mabingwa katika miaka ya 2002, 2003, 2005, 2011, 2012, 2017, 2018, 2019, 2020, na 2023.

Wakati huo huo, Yanga, mabingwa wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita, ni kama wameendeleza ubabe wao kwa Simba katika mechi za Ngao ya Jamii. 

Kuanzia mwaka 2021, timu hizo zimekutana mara sita (ikiwamo ya leo) katika Ngao ya Jamii. Yanga imeshinda tano na ya mwisho ikiwa ni ile ya Septemba 16, 2025, ambapo iliifunga Simba bao 1-0.

Related articles

Recent articles