30.4 C
New York

Vichocheo vya kufikia malengo ya Dira 2050: Sayansi na Teknolojia

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

SAYANSI na Teknolojia zinachochea ubunifu na kuongeza tija na ushindani. Hivyo basi, sayansi na teknolojia ni vichocheo muhimu vinavyoleta tija, ufanisi na ukuaji endelevu wa uchumi.

Ni kwa maana hiyo, hakuna namna maendeleo ya sayansi na teknolojia yanavyoweza kutofautishwa na ustawi wa jamii au taifa kwa ujumla.

HATUA ZILIZOPIGWA

Tanzania, kama zilivyo nchi nyingi duniani, imepiga hatua kubwa katika matumizi ya sayansi na teknolojia, ikilenga kuongeza ufanisi, ubora wa upatikanaji wa huduma na kuimarisha uzalishaji.

Hatua hizo ni pamoja na uwekezaji katika sekta ya nishati, ikiwamo matumizi ya nishati mbadala ya jua na bayogesi ili kukidhi mahitaji na kuongeza kasi ya maendeleo, hasa maeneo ya vijijini.

Kwa upande mwingine, bayoteknolojia imeendelea kutumika kwa upana katika sekta za kilimo, utalii, madini, mifugo, elimu, afya, na viwanda, ikilenga kuongeza uzalishaji na ufanisi.

Pia, matumizi ya bayoteknolojia yamewezesha kupunguza gharama na kuimarisha ushindani wa kiuchumi, kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi.

CHANGAMOTO

Licha ya mafanikio hayo, bado kuna ukosefu wa miundombinu, upungufu wa fedha, ukosefu wa ujuzi wa kutosha kulingana na mahitaji, ushirikiano mdogo baina ya wadau, na kukosekana kwa mipango thabiti inayorahisisha uingizaji wa teknolojia kutoka nje (nchi zilizoendelea).

Vilevile, kuna changamoto ya kukosekana kwa usawa katika upatikanaji wa elimu bora kwa masomo ya hisabati, sayansi, na teknolojia kati ya wanawake na wanaume.

Sambamba na hilo, ipo changamoto ya kutokuwepo kwa jitihada madhubuti zinazolenga ugunduzi wa mapema wa vipaji kwa watoto.

MATARAJIO

Kufikia waka 2050, Tanzania inatarajiwa kuwa na ongezeko la matumizi ya teknolojia za kisasa katika ngazi zote za uzalishaji na utoaji wa huduma ili kuongeza ufanisi na kuchochea mabadiliko.

Pili, Tanzania kuwa na vituo vya ubunifu na maeneo mahususi yenye hadhi ya kimataifa kwa ajili ya tafiti na uvumbuzi katika sekta muhimu za kilimo, viwanda na afya, vikiwa na wataalamu mahiri na rasilimali za kutosha kukidhi mahitaji ya ndani.

Tatu, kuwa na jamii inayotumia teknolojia za kisasa zinazohusisha na kukidhi mataji ya watu wenye ulemavu, kwa kuzingatia mifumo inayowapa fursa ya kushiriki kikamilifu na kuchangia katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Nne, kuwa na taasisi imara zinazofuatilia na kufanya tathmini ya taarifa za maendeleo ya kiteknolojia ili kuiandaa nchi kuwa tayari kutumia teknolojia kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kuimarisha ushindani.

Tano, kuwa na mfumo jumuhishi unaokuza masomo na matumizi ya sayansi, teknolojia, uhandisi, na hisabati, ukiwa na lengo la kutoa fursa sawa na kuwawezesha wanawake na wasichana kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kisayansi na ubunifu.

Sita, kuwa na uwekezaji thabiti na jumuhishi katika kukuza na kutumia teknolojia zinazoibuka ili kusaidia viwanda na kukuza maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Related articles

Recent articles