27.5 C
New York

Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Zambia

Published:

LUSAKA, Zambia

UCHAGUZI Mkuu nchini Zambia utafanyika Alhamisi ya wiki hii, yaani Agosti 13, 2026, na macho ya wengi yameeelekezwa katika kinyang’anyiro cha urais.

Ifahamike kuwa Rais wa sasa, Hakainde Hichilema, anawania muhula wake wa pili na akikabiliana na wagombea wengine 13.

Wananchi takribani milioni 8.7, wengi wao wakiwa ni wanawake na vijana wenye umri kati ya miaka 18 na 35, wanatarajiwa kupiga kura Alhamisi.

Matokeo ya urais yatatangazwa Agosti 17, 2026, kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi. Mgombea atalazimika kufikisha asilimia zaidi ya 50 ya kura ili kutangazwa kuwa Rais mpya.

Wakati huo huo, Uchaguzi wa mwaka huu utashuhudia pia ongezeko la idadi ya wabunge; kutoka 156 hadi 226.

RAIS V WAZIRI

Licha ya kuwapo kwa wagombea wa urais 14, ushindani mkali upo kwa Hichilema na Brian Mundubile wa National Republican Party
(NRPUP), ambaye aliwahi kuwa Waziri na mshirika wa kiongozi wa zamani wa Taifa hilo, Edgar Lungu (sasa marehemu).

Hichilema, kiongozi wa Chama cha United Party for National Development (UPND), aliingia madarakani baada ya ushindi katika Uchaguzi wa mwaka 2021. Ni baada ya kukosa urais katika chaguzi tano za awali.

Mundubile (65), anajivunia uungwaji mkono kutoka ndani ya Chama cha Lungu, Patriotic Front, ambacho kina nguvu kubwa maeneo ya Kaskazini na Mashariki mwa Zambia.

HIZI HAPA CHANGAMOTO

Katika muhula wake wa kwanza, Hichilema mwenye umri wa miaka 64 anapongezwa kwa namna alivyoshughulika na madeni ya nchi hiyo kwa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

Pia, ukuaji wa uchumi wa Zambia ni eneo jingine ambalo Hichilema amepongezwa mara kadhaa na jumuhiya za kimataifa na hata wawekezaji.

Lakini, kwa wananchi, malalamiko ya walio wengi ni kwamba maisha yao hayabebi picha ya sifa hizo za uchumi wa nchi kukua.

Vilio ni vingi juu ya kupanda kwa bei ya vyakula, uhaba wa ajira, na kiwango kikubwa cha umasikini, ambapo asilimia 70 ya raia wanaishi chini ya kipato cha Dola tatu za Marekani kwa siku.

“Duniani kote, zipo sifa kuwa tunafanya vizuri (kiuchumi) lakini (Hichilema) anatakiwa kulifanya hilo lionekane pia hapa nyumbani,” anasema Semi Malama (26), ambaye ni mwanafunzi wa masuala ya afya.

Kwa Afrika, Taifa hilo la Kusini mwa Afrika linashika nafasi ya pili kwa uzalishaji mkubwa wa madini ya shaba na mpango wa Serikali ni kuzidisha mara tatu kiwango cha sasa ifikapo mwaka 2031.

SURA YA UCHAGUZI

Kampeni zilishuhudia vurugu na hata vitisho, hasa kwa vyama vya upinzani. Itakumbukwa, NRPUP kilizishutumu mamlaka kwa kuingilia kampeni zake mara kadhaa.

Wakati huo huo, polisi walitumia mabomu ya machozi katika baadhi ya mikutano ya kampeni. Wiki iliyopita, mmoja ya viongozi wa upinzani alidai kuwa wadunguaji walikuwapo katika moja ya mkutano wao mjini Mongu, takribani kilometa Magharibi mwa Lusaka.

Related articles

Recent articles