CARACAS, Venezuela
SIKU chache zilizopita, Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela, Felix Plasencia, alitangaza uamuzi wa nchi hiyo kuondosha uanachama wake katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).
Kwa mujibu wa Plasencia kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X, zamani ukifahamika kwa jina la Twitter, hatua ya kujitoa ICC ni maelekezo ya Rais wa mpito, Delcy Rodriguez.
Kwa upande mwingine, Venezuela kujitoa ICC kunatafsiriwa kuwa ni mwelekeo mpya wa nchi hiyo katika sera za kimataifa, ingawa wapo wanaoamini imeifuata maelekezo ya Marekani.
Marekani, ambayo imekuwa na ushawishi mkubwa katika siasa za Venezuela tangu ilipomng’oa madarakani Rais Nicolas Maduro, ilikuwa ya kwanza kuipongeza Venezuela kwa hatua hiyo.
Akiutaja uamuzi huo kuwa ni sahihi, Plasencia alisema kwa miaka mingi ICC imekuwa ikiendeshwa kwa misingi ya upendeleo kwa kuzikandamiza nchi za Afrika na Latin ya Amerika.
Inafahamika kuwa Marekani si sehemu ya wanachama na imekuwa ikikosoa utendaji kazi wa Mahakama hiyo kwa madai kuwa imekuwa ikiiminya na kupendelea maadui zake.
Katika kuipongeza Venezuela, Serikali ya Marekani ilidai kuwa ICC ilitumia miaka mingi kumchunguza Maduro lakini haikuwahi kuja na ushahidi wa madudu yake.
Aidha, Marekani katika taarifa yake hiyo ilienda mbali zaidi na kuzitaka nchi zingine zilizo na uachama wa ICC kujitoa kama ilivyofanya Venezuela.
Hata hivyo, ICC imeweka wazi kuwa Vezuela kutangaza kujitoa hakumaanishi kwamba itaacha kuchunguzwa juu ya vitendo vyake vya uhalifu dhidi ya binadamu.
Ni kwa mujibu wa Mkataba wa Roma ulioasisi ICC, kwamba itachukua mwaka mmoja kwa nchi iliyowasilisha ombi la kujitoa kuhesabika si sehemu ya Mahakama hiyo.
Hivyo basi, kama kuna uchunguzi uliokwishaanza kabla ya kujitoa, utaendelea na washitakiwa kuhukumiwa. Uchunguzi wa ICC dhidi ya Venezuela ulianza mwaka 2021.
Uchunguzi ulilenga kubaini kama kulikuwa na vyombo vya dola na wakosoaji wa Serikali walihusika katika vitendo vya uhalifu dhidi ya binadamu wakati wa maandamano ya mwaka 2017.
Kama itakumbukwa, uhusiano wa ICC na Venezuela uliyumba zaidi Januari, 2025, baada ya Mahakama hiyo kufunga ofisi yake nchini humo.
Uamuzi huo wa ICC ulitokana na madai yake, kwamba Serikali ya Venezuela haijachukua hatua zozote za maana katika kuchunguza madai ya uhalifu.
Desemba, 2025, ndipo Bunge la Venezuela lilipopiga kura ya kuanza mchakato wa kujitoa katika Mahakama hiyo, hatua iliyotafsiriwa kuwalinda viongozi wa Serikali dhidi ya mashitaka ya ICC.
Juu ya madai ya ICC kupendelea baadhi ya nchi, wakati fulani nadharia hiyo ilionekana kuwa na ukweli baada ya viongozi wengi wa Afrika kufunguliwa mashitaka.
Lakini, kwa miaka ya hivi karibuni, hata ‘wakubwa’ kama Rais wa Urusi, Vladimir Putin, na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, wameshitakiwa kwa nyakati tofauti.
Putin anatajwa na ICC katika kile kinachoendelea kati ya Urusi na Ukraine, wakati Netanyahu anashutumiwa kwa uhalifu dhidi ya binadamu kwenye vita vya Israel na Palestina huko Gaza.
Katika hatua nyingine, Serikali ya Chad nayo imetangaza mpango wake wa kujitoa ICC, sababu zikiwa ni zilezile, Mahakama hiyo kuwashughulikia zaidi viongozi wa nchi za Afrika.
Chad imedai kuwa kati ya mashitaka 13 yaliyowahi kufunguliwa na ICC tangu kuanzishwa kwake, tisa yanawahusu viongozi wa Afrika, jambo linalotosha kuthibitisha uonevu wa Mahakama hiyo.
Wakati huo huo, Chad iliweka wazi kuwa uamuzi wake umetokana na ushawishi wa Marekani iliyotaka kutafakari uanachama wake ndani ya ICC.
“Marekani ilieleza shaka yake juu ya utendaji kazi wa Taasisi hiyo na kuitaka Chad kujitafakari juu ya uanachama wake katika Mkataba wa Roma,” ilieleza taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Chad.
Kabla ya Chad, tayari Burkina Faso, Mali na Niger, ambazo kimsingi ziko chini ya tawala za kijeshi, zilijitoa ICC tangu mwaka 2025.
ICC inakumbwa na dhoruba hilo zikiwa ni siku chache tu zimepita tangu Mahakama hiyo ilipompoteza Mwendesha Mashitaka Mkuu wake,
Karim Khan, ambaye alipigiwa kura za kung’olewa baada ya kukumbwa na kashfa za unyanyasaji wa kingono dhidi ya msaidizi wake.


