RIO, Brazil
KWA mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa kupitia Programu yake ya Ukimwi (UNAIDS), watu zaidi ya milioni tatu watakuwa na maambukizi ya ugonjwa huo kufikia mwaka 2030.
Katika ripoti yake ya hivi karibuni, watu milioni 1.2 walipata maambukizi mwaka 2025, huku wengine 570, 000 wakipoteza maisha.
UNAIDS imeeleza kuwa hali imekuwa mbaya baada ya baadhi ya wafadhili wa kimataifa, ikiwamo Marekani, kusitisha misaada ya kuwezesha mapambano dhidi ya Ukwimi.
Mathalan, huduma za kujikinga na Ukimwi katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara zilitegema ufadhili wa nje kwa asilimia 80.
Mbaya zaidi, watu milioni tisa kati ya 41 wanaoishi na virusi vya Ukwimi duniani hawapo kwenye mfumo wa tiba, jambo linaloashiria kuongezeka kwa maambukizi.
Kama hiyo haitoshi, nusu ya watoto wenye maambukizi hawajawezeshwa na huduma ya dawa za kudhibiti maambukizi kwa wengine, kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2025.
Kwa upande mwingine, nchi saba duniani zimeonesha kupiga hatua kubwa na kupunguza asilimia takribani 80 ya maambukizi mapya kuanzia mwaka 2010.
Hata hivyo, kinga dhidi ya Ukimwi haijafanikiwa vya kutosha kufika maeneo mengi duniani. UNAIDS inatazamia ziwafikie watu milioni 20. “Mafanikio siyo kugundua (kinga), bali ziweze kuwafikia watu,” inasisitiza ripoti hiyo.
Brazil imeonesha kupiga hatua kubwa katika eneo hilo, ambapo kiwango cha ufikishaji wa dawa za kinga ya Ukimwi kwa watu wake kimepanda kwa asilimia 41.
Lakini, hatua ya baadhi ya nchi kupiga marufuku biashara ya ukahaba na mapenzi ya jinsia moja nazo zimetajwa kufifisha jitihada za kukabiliana na Ukimwi duniani.
Burkina Faso na Niger zilifanya hivyo mwaka 2025. Mwaka huu, nchi 168 zilipiga marufuku ukahaba na 66 zilikataza mapenzi ya jinsia moja.
Kwa wanaharakati wa masuala ya afya, hii inaibua hofu kwa watu wa makundi hayo kujitokeza kwenye huduma za kinga au tiba za Ukimwi, hali inayoweza kuchochea maambukizi zaidi.


