29.4 C
New York

Usiyoyajua kuhusu mkasa wa bilionea wa Telegram

Published:

LOS ANGELES, Marekani

BILIONEA anayemiliki mtandao wa kijamii wa Telegram, Pavel Durov, anakabiliwa na shutuma kutoka katika mataifa mawili ya Urusi na Ufaransa.

Katika taarifa yake ya jana Julai 29, 2026, Idara ya Usalama ya Urusi (FSB) ilimtuhumu Durov kwa kufadhili shughuli za kigaidi, ikisisitiza kuwa itamuweka kwenye orodha ya wahalifu wanaotafutwa.

Hata hivyo, hilo halikuonekana kumtisha raia huyo wa Urusi mwenye umri wa miaka 41, na badala yake alitumia akaunti yake ya X kuposti picha inayomuonesha akionesha kidole cha kati.

Kwa mujibu wake, mamlaka za Urusi zinajaribu kuufungia mtandao wake wa Telegram ili kuendeleza uminyaji wa uhuru wa kujieleza na kutoa maoni.

Kwamba mamlaka zinabana uhuru wa wananchi kueleza walivyochoka kiuchumi kutokana na vita vya miaka minne kati ya Taifa hilo na Ukraine.

Durov alizaliwa mjini Leningrad, sasa ukifahamika kwa jina la St. Petersburg, na anamiliki pia uraia wa nchi zingine tatu; Ufaransa, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na St. Kitts and Nevis.

Akiwa na umri wa miaka 22 mwaka 2006, Durov na kaka yake, Nikolai, walianzisha VKontakte, ambao ni mtandao wa kijamii mkubwa zaidi Urusi kama ilivyo Facebook.

Wakati wa maandamano makubwa ya kupinga Serikali ya mwaka 2011 hadi 2012, mtandao huo uliingia kwenye mgogoro na mamlaka, kiasi cha Durov kulazimika kuuza hisa zake.

Mwaka 2013, ndipo Durov na Nikolai walipoanzisha mtandao mwingine wa Telegram lakini halikuchukua muda mrefu kabla ya kukamatwa nchini Ufaransa.

Kwa upande wa Ufaransa, mamlaka za nchi hiyo zinautaja mtandao wake huo kutumiwa na wahalifu kuratibu vitendo vya utakatishaji fedha, usafirishaji wa dawa za kulevya na usambazaji wa picha na video za ngono kwa watoto.

Mwaka 2024, Durov alikamatwa na vyombo vya dola jijini Paris. Aliachiwa siku nne baadaye baada ya kulipa euro milioni tano kama dhamana. Mwaka uliofuata, baada ya mivutano mingi na Serikali, aliondoka Urusi na kuhamia Dubai.

Katika mahojiano yake ya mwaka 2024, Durov mwenye utajiri wa Dola bilioni 6.6 alisema Dubai ni sehemu salama zaidi kwa mitandao ya kijamii kama wake, ujumbe uliotafsiriwa kuwa ni ‘dongo’ kwa Serikali ya Urusi.

Tajiri huyo ana watoto sita katika mahusiano yake na wanawake watatu. Wakati fulani, alidai kuchangia mbegu za uzazi katika nchi 12.

Telegram ni moja ya mitandao ya kijamii yenye ushawishi mkubwa, ukiripotiwa kuwa na watumiaji zaidi ya bilioni moja kwa mwezi duniani kote.

Related articles

Recent articles