Na mwandishi wetu, Gazetini
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Emmanuel Nchimbi, amewataka Watanzania kuendelea kudai kupatikana kwa Katiba mpya yenye maridhiano ya kitaifa, akisema ndiyo msingi wa kuimarisha haki za binadamu, utawala bora na demokrasia nchini.
Akizungumza wakati wa kufungua Mkutano Mkuu wa 15 wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) jijini Dar es Salaam, Ijumaa, Dk. Nchimbi alisema iwapo angepewa nafasi ya kuwaambia Watanzania jambo moja tu, angewasihi kupigania upatikanaji wa Katiba mpya.
“Pambaneni mpate Katiba mpya yenye makubaliano ya wadau wote, Katiba yenye muafaka katika taifa, Katiba itakayotupeleka mbele katika miaka 50 ijayo na ambayo kila Mtanzania atajivunia kwa sababu inajali maisha ya watu na kuheshimu haki za raia wake,” amesema.
Kauli hiyo inakuja wakati mjadala kuhusu Katiba mpya ukiendelea nchini. Mchakato wa kuandika Katiba mpya ulianza mwaka 2011 chini ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete, lakini ukasimama mwaka 2014 kabla ya kufikia hatua ya kura ya maoni. Rais Samia Suluhu Hassan ameahidi kuwa mchakato huo utaendelezwa kabla ya mwaka 2030, huku Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 pia ikiahidi kuufufua.
Dkt. Nchimbi alisema haki za binadamu haziishii kwenye sheria na mahakama pekee, bali zinahusu maisha ya kila siku ya wananchi.
“Haki ni mama anayetaka mtoto wake awe salama, ni baba anayetaka kulisha familia yake kwa heshima, ni kijana anayetaka kusikilizwa, ni mwananchi anayetaka kutoa maoni yake bila hofu, ni mtuhumiwa anayestahili kutendewa kwa mujibu wa sheria, ni polisi anayekwenda kazini akitarajia kurudi salama kwa familia yake na ni mwandishi wa habari anayetaka kufanya kazi yake. Hata kama hana cheo, hana fedha wala mtu wa kumsemea, bado ana utu na kwa sababu ana utu ana thamani. Hapo ndipo haki za binadamu zinapoanzia,” amesema.
Amesisitiza kuwa pamoja na kuwepo kwa madai mengi kutoka kwa makundi mbalimbali ya jamii, msingi wa kuyapatia suluhisho la kudumu ni kuwa na Katiba inayokubalika na Watanzania wote.
“Ukisikiliza madai ya makundi mbalimbali, utakuta yapo mengi kwa wakati mmoja. Lakini lazima uchague jambo kubwa linalobeba yote. Jambo hilo ni Katiba,” amesema.


