LONDON, Uingereza
WAKATI ikiwapo dhana kuwa wafanyabiashara wakubwa wamekuwa na kawaida ya kukwepa kodi za serikali katika nchi zao, kwa Uingereza imekuwa tofauti.
Kundi la mamilionea 120 limemwandikia barua Waziri Mkuu mpya, Andy Burnham, likimuomba kuwaongezea malipo ya kodi ili kuimarisha uchumi wa nchi hiyo na kuwasaidia wananchi wengine.
Ombi lao hilo limekuja wakati tayari Serikali chini ya Waziri Mkuu huyo ikiwa imetangaza asilimia 2 ya kodi kwa kila tajiri anayemiliki zaidi ya Pauni milioni 10.
Sasa, katika orodha hiyo ya matajiri walioomba walipe zaidi ya hapo, yumo mwanasoka wa zamani wa Ligi Kuu ya England, ambaye sasa ni mtangazaji nyota wa vipindi vya televisheni, Gary Lineker.
Lineker aliwahi kuwa mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) anayelipwa zaidi (Pauni milioni 1.3 kwa mwaka). Kwa sasa utajiri wake ni Pauni milioni 30.
Wakati huo huo, katika matajiri hao, yamo pia majina ya mwigizaji wa filamu wa kike, Julia Davies, pamoja na prodyuza maarufu wa muziki, Brian Eno.
“Tukiwa kama mamilionea, tuna ujumbe kwa ajili yako Waziri Mkuu wetu mpya. Tutoze kodi zaidi. Tunajivunia kulipa kodi,” inasomeka sehemu ya barua yao hiyo.
Matajiri hao wanaojiita ‘Mamilionea Wazalendo’, wamesema kwa miaka mingi utajiri umekuwa ukimilikiwa na wachache, hivyo kuumiza nchi, watu, demokrasia na mazingira.
“Tunamudu kulipa. Hatuzungumzii kuongeza kodi kwa watu wanaomka asubuhi kwenda kutafuta kipato cha siku. Tunazungumzia matajiri,” inaeleza barua yao kwa Waziri Mkuu.
Pia, wamesema hatua yao hiyo imelenga kuleta mabadiliko, ikizingatiwa kuwa fedha watazokatwa kama kodi ya ziada zitaimarisha miundombinu ya umma na kuwezesha biashara ndogondogo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Hazina, Emma Reynolds, amesema anawaalika matajiri wengine wanaotaka kutozwa kodi zaidi. “Nawakaribia wenye mioyo ya kutoa zaidi. Wanaweza kulipa (kodi) zaidi,” amesema.


