LAGOS, Nigeria
MAHAKAMA nchini Nigeria imewahukumu kifungo cha maisha jela wanaume watatu baada ya kupatikana na hatia ya makosa yanayohusiana na utekaji wa makumi ya wanafunzi na walimu katika Jimbo la Oyo, kusini-magharibi mwa nchi.
Watuhumiwa hao walikiri kuficha taarifa muhimu kuhusu wahusika wa mashambulizi dhidi ya shule pamoja na kukubali kuwa wanahusishwa na kundi la Boko Haram, ambalo limekuwa likihusishwa na mashambulizi ya kigaidi na utekaji wa raia nchini humo.
Hukumu hiyo imetolewa takribani wiki mbili baada ya mamlaka za Nigeria kutangaza kuokolewa kwa wanafunzi na walimu 44 waliotekwa nyara wakati wa mashambulizi yaliyoratibiwa dhidi ya shule tatu katika Wilaya ya Oriire mwezi Mei mwaka huu.
Mashambulizi hayo yalizua hofu kubwa nchini Nigeria na kuchochea maandamano kutoka kwa wazazi, vyama vya walimu na wanaharakati wa haki za binadamu waliotaka serikali kuongeza ulinzi katika shule na maeneo mengine muhimu ya huduma za jamii.
Katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita, utekaji wa watu kwa lengo la kudai fedha za fidia umegeuka kuwa moja ya changamoto kubwa za kiusalama nchini Nigeria. Makundi yenye silaha yamekuwa yakivamia shule, vijiji, makanisa na misikiti katika maeneo yenye ulinzi hafifu, yakiteka mamia ya watu na kudai malipo ili kuwaachia huru.
Licha ya operesheni zinazoendelea kufanywa na vikosi vya usalama, Nigeria bado inakabiliwa na vitisho kutoka kwa makundi mbalimbali yenye silaha, yakiwemo magenge ya wahalifu yanayofahamika kama “bandits”, ambayo hujihusisha na uporaji, utekaji na mauaji.
Mbali na tatizo hilo, nchi hiyo pia inaendelea kukabiliana na uasi wa makundi ya wanamgambo wa Kiislamu, migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji pamoja na harakati za makundi yanayotaka kujitenga katika baadhi ya maeneo, hali inayozidi kuifanya changamoto ya usalama kuwa kubwa zaidi.


