28.7 C
New York

ICC yakomalia uhalifu dhidi ya binadamu Sudan

Published:

HAGUE, Uholanzi

MAHAKAMA ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC) imeendelea kulaani kinachoendelea Sudan, ikisema upo ushahidi wa uwepo wa matukio ya uhalifu dhidi ya binadamu katika vita vinavyoendelea nchini humo.

Mmoja ya vigogogo wa ICC, Nazhat Shameem Khan, amesema Mahakama hiyo imejiridhisha kuwa vitendo hivyo vimeshika kasi katika miji ya el-Fasher na el-Geneina.

“Inaweza kuchukua muda kwa haki kupatikana lakini tutafanikisha tu,” amesema Khan na kuwataja wapiganaji wa RSF kuwa ndiyo wahusika wakuu wa vitendo vya uhalifu dhidi ya binadamu.

El-Fasher ni moja ya miji yenye kiwango kikubwa cha mauaji katika vita vinavyoendelea kati ya wapiganaji wa RSF na wanajeshi wa Serikali.

Makundi hayo mawili yamekuwa kwenye uwanja wa vita tangu mwaka 2023, chanzo kikiwa ni kugombea madaraka, kila moja likitaka kuiongoza Sudan.

Takwimu za Umoja wa Mataifa (UN) zinaonesha kuwa watu zaidi ya 6,000 waliuawa wakati RSF ilipoteka Mji huo Oktoba, 2025.

Khan amesema tayari ICC ina ushahidi wa kutosha wa namna viongozi wa RFS walivyohusika na kinachosubiriwa ni kuwafikisha mbele ya Mahakama hiyo kwa ajili ya kujibu mashitaka.

“Hatuwezi kusema itachukua muda gani lakini tunasisitiza kuwa maendeleo ni mazuri na tumefikia hatua nzuri,” amesema Khan.

ICC yenye makao makuu yake nchini Uholanzi, ni Mahakama ya Kimataifa yenye mamlaka ya kufunga mashitaka dhidi ya wahusika wa mauaji ya halaiki, uhalifu wa kivita, na uhalifu dhidi ya binadamu.

Kwa upande wake, RSF imekana mara kadhaa kuhusika katika makosa hayo, licha ya kukiri kuwapo kwa mauaji, hasa katika Mji wa el-Fasher.

Kundi hilo linadhibiti sehemu kubwa ya Magharibi mwa Sudan, huku maeneo mengine yakiwa chini ya jeshi na vikundi vingine vya waasi.

Related articles

Recent articles