28.7 C
New York

‘Mende’ wa India wanavyompasua kichwa Waziri Mkuu

Published:

NEW DELHI, India

MAANDAMANO makubwa ya vijana nchini India yanaipa wakati mgumu Serikali ya Waziri Mkuu, Narendra Modi.

Gen-Z hao kupitia Chama chao cha ‘Vijana wa Mende’ (CJP) wameingia barabarani na maandamano yao yamesababisha majeruhi zaidi ya 200, wakiwamo polisi.

Kutokana na kasi na ukubwa wa maandamano hayo, Serikali ililazimika kuzima mtandao katika maeneo mengi ya Mji Mkuu wa Delhi.

Chanzo cha kujiita Mende ni kauli ya mmoja ya viongozi wa Serikali aliyewafananisha na mdudu huyo vijana wasio na ajira, akisema ni wavivu na wasiojituma.

Aidha, chanzo cha maandamano ni hatua ya Wizara ya Elimu kufuta mitihani ya usajili wa kuingia taaluma ya afya baada ya kubaini kuwa maswali yalishavuja.

Hatua hiyo iliathiri mamilioni ya wanafunzi, hivyo kuungana na kuanzisha maandamano ya kushinikiza Waziri wa Elimu, Dharmendra Pradhan, ajiuzulu.

Wakati huo, hakukuwa na Chama cha Mende, bali vijana tu, wengi wao wakiwa ni wanafunzi, waliandamana kupaza sauti juu ya kilichotokea (mtihani kufutwa).

Baadaye, jina la Mende lilianza kupata umaarufu mitandaoni, vijana wakilitumia kama nembo yao kwa kile alichokisema kiongozi.

Vijana wasio na ajira na waliochoshwa na ugumu wa maisha, wakiwamini kwa kiasi kikubwa hali yao hiyo imesababishwa na hao wanaowaita mende.

Hasira za vijana ziliongezeka mara dufu baada ya mwanaharakati Sonam Wangchuk kukimbizwa hospitali akiwa kwenye hali mbaya baada ya kugoma kula kwa wiki tatu akiwa gerezani anakoshikiliwa.

Kwa wiki za hivi karibuni, Mende wameonekana kuvuna ushawishi hata kwa wanasiasa wa upinzani, akiwamo Mbunge wa Chama cha Congress, Renuka Chowdhury.

Chowdhury ameibuka na kuitupia lawama Serikali ya Mondi, akilaani nguvu kubwa inayotumiwa na vyombo vya dola katika maandamano ya vijana.

“Hivi ndivyo Serikali inapaswa kufanya? Kutumia mabomu ya machozi na risasi dhidi ya wanafunzi? Serikali hii haina maana yoyote,” amesema Chowdhury.

Hata hivyo, hii si mara ya kwanza kwa India kuingia kwenye maandamano yaliyotikisa nchi.

Mwaka 2011, vuguvugu la kupinga vitendo vya rushwa serikalini (AIC) likiongozwa na mwanaharakati Anna Hazare liliingiza mamilioni ya raia barabarani.

Miaka 10 baadaye, yaliibuka maandamano mengine makubwa ya wakulima wakipinga sheria walizodai kuwakandamiza.

Mwisho, wachambuzi wa siasa wanasema licha ya uchanga wa CJP, kinameweza kuungwa mkono na makundi yote katika jamii, tofauti na AIC na hata maandamano ya wakulima.

Hata hivyo, bado wengi wao ni watu wa mijini, tofauti na Chama tawala, Bharatiya Janata Party (BJP), ambacho kimejenga msingi mzuri na wa muda mrefu katika maeneo mengi ya vijijini.

Related articles

Recent articles