LOS ANGELES, Marekani
BONDIA wa ngumi za uzito wa juu ambaye pia ni mshindi wa medali ya dhahabu katika michuano ya Olimpiki, Anthony Joshua, atapanda ulingoni Julai 25, 2026.
Joshua, bingwa wa dunia mara mbili, atavaana na Kristian Prenga na pambano hilo litapigwa mjini Riyadh, Saudi Arabia.
Je, ni nani huyo Prenga? Ni raia wa Albania aliyezaliwa Januari 24, 1991. Kwa sasa amehamishia makazi yake mjini New Jersey, Marekani.
Prenga (35), alianza kucheza ngumi alipokuwa gym kwa ajili ya kupunguza uzito. Alianzia katika ‘kick box’ (ngumi na mateke), ambapo alitwaa mkanda wa Ulaya wa IKBF.

Baadaye, ndipo ‘Eagle’ akahamia kwenye mchezo wa ngumi usiohusisha mateke (boxing). Tofauti na mabondia wengi, hakuanzia kwenye ridhaa, aliingia moja kwa moja kwenye ngumi za kulipwa.
Katika pambano lake la kwanza tu, Mei, 2016, alimaliza ndani ya dakika dakika 4, akimpiga kwa KO ya raundi ya pili bondia Pavel Siska mjini Munich, Ujerumani.
Machi, 2023, Prenga alitwaa mkanda wa Chama cha Ngumi cha Amerika ya Kaskazini (NABA) kwa kumdunda Samuel Crossed kwa KO ya raundi ya tatu.
Tangu aingie kwenye ngumi za kulipwa, ameshinda mapambano 20, yote kwa KO; mara saba kwa KO ya raundi ya kwanza na mara saba katika raundi ya pili.
Kwa sasa, ni miongoni mwa mabondia wanaofanya vizuri kwa mauzo ya tiketi mjini New Jersey. Amepigana katika nchi tano tofauti lakini Julai 25, 2026 itakuwa mara yake ya kwanza kwenda Saudia.
Kwa Albania, anashika nafasi ya pili kwa ubora, nyuma ya Nelson Hysa, ambaye ameshinda mapambano yake yote 24, akishinda 22 kwa KO.
Katika mahojiano yake kadhaa, Prenga mwenye urefu wa futi 6 na inchi 5 amekuwa akiwataja Evander Holyfield na Lennox Lewis kuwa ndiyo mabondia anaowakubali.
Kuelekea Julai 25, Prenga amesema: “Anthony Joshua ni bondia mzuri lakini kosa alilofanya ni kunichagua mimi niwe mpinzani wake. Hili ni pambano linalokwenda kubadilisha maisha yangu na yake.
“Najua wana mipango mingi baada ya pambano hili. Najua wananichukulia poa. Nafurahia kuona hilo, ila nitatibua mipango yao na kuishangaza dunia Julai hii huko Saudi Arabia,” amesema.


