ROMA, Italia
KANISA Katoliki lina wafuasi bilioni 1.4 duniani kote, hivyo kulifanya kuwa moja ya taasisi zenye nguvu na ushawishi mkubwa.
Kama zilivyo taasisi zingine, Kanisa Katoliki limekuwa na taratibu zake, zikiambatana na adhabu endapo zitakiukwa.
Ndicho kilichotokea. Uongozi wa Kanisa hilo lenye Makao Makuu yake mjini Vatican umechukua hatua kali za kinidhamu dhidi ya maaskofu sita.
Hatua ya kuwatenga maaskofu hao, akiwamo Askofu wa Hispania, Alfonso de Galarreta, ilitangazwa jana Julai 2, 2026, mjini Vatican.

CHANZO CHA HUKUMU
Adhabu kwa maaskofu hao wa Jumuhiya ya Mtakatifu Pius X (SSPX) ya Uswis imekuja baada ya kitendo chao cha kuidhinisha ibada za Sakramenti bila idhini ya Papa Leo XIV.
Bila idhini ya Kiongozi huyo wa Vatican, maaskofu wawili, akiwamo Galarreta wa Hispania, waliongoza ibada ya kuwekwa wakfu maaskofu wanne wapya; Pascal Schreiber (Uswis), Michael Goldade (Marekani), na Michel Poinsinet de Sivry na Marc Hanappier (Ufaransa).
MAMLAKA YA PAPA
Inafahamika kwa Papa pekee ndiye mwenye mamlaka ya kuidhinisha kuwekwa wakfu kwa maaskofu wapya, hivyo kilichofanyika Uswis ni kukiuka utaratibu huo.
Hata hatua ya Kanisa Katoliki kuwaadhibu maaskofu hao ilitanguliwa na barua aliyoandika Papa Leo XIV kwa Padri Mkuu wa Jumuhiya ya Mtakatifu Pius X, Davide Pagliarani.
TAMKO KUTOKA USWIS
Baada ya maaskofu wake sita kushukiwa na rungu, Jumuhiya ya Mtakatifu Pius X imekiri kusikitishwa na kilichotokea.
Kwa mujibu wa Padri Pagliarani, hawaungi mkono kilichofanywa na maaskofu hao, na badala yake wanamuheshimu Papa na mamlama aliyonayo kama kichwa cha Kanisa Katoliki duniani.
”… Kwa sababu tunampenda Mwakilishi wa Yesu Kristo, ndiyo sababu hatutaki tena kuona aibu hii kwa Papa,” amesema Padri Pagliarani.
CHIMBUKO, UTATA WA SSPX
Mtakatifu Pius X ni Jumuhiya iliyoasisiwa na Askofu Mkuu raia wa Ufaransa, Marcel Lefebvre, katika miaka ya 1970.
Askofu Lefebvre alifanya hivyo baada ya kutokuridhishwa na mabadiliko yaliyofanyika Vatican katika miaka ya 1960, akiamini yalikiuka mafundisho na imani ya Kikatoliki.
Baadhi tu ya hayo aliyopingana nayo ni Kanisa Katoliki kubadilisha uhusiano wake na madhehebu mengine, pamoja na lugha mbalimbali kutumika kuadhimisha Misa.
Kwa upande wake, SSPX ilibaki kutambua na kutumia Kilatini kama lugha ya Misa na tangu hapo imekuwa na uhusiano usio na afya kati yake na Kanisa Katoliki.
Hii si mara ya kwanza kwa maaskofu wake kupigwa pini na Kanisa Katoliki. Katika miaka ya 1980, maaskofu wake walitengwa kwa kosa la kutokuheshimu mamlaka za Vatican, ingawa baadaye walisamehewa.
Kwa sasa, Jumuhiya hiyo ina maaskofu sita, mapadri 751, wafuasi zaidi ya 600,000 na ina uwakikishi katika nchi 50 duniani.


