37.6 C
New York

Drake kwa ‘kubeti’ humwambii kitu

Published:

TORONTO, Canada

NJE ya kazi ya muziki, rapa Drake ana dunia yake nyingine. Ni miongoni mwa ‘walevi’ wa kamari ya kubashiri matokeo ya michezo (kubeti).

Hivi karibuni, supastaa huyo wa Hip hop mzaliwa wa Toronto, Canada, alivuna Dola za Marekani milioni moja (zaidi ya Sh bil. 2.6 za Tanzania).

Ni baada ya kupatia katika ubashiriki wake wa mechi ya hatua ya 32 Bora ya fainali za Kombe la Dunia kati ya Canada na Afrika Kusini kwenda vizuri.

Katika mchezo huo, Drake alibashiri kuwa ‘chama’ lake la nyumbani, Canada, lingeibuka na ushindi na ndicho kilichotokea. Bafana Bafana ‘walifungwa’ bao 1-0.

Drake aliweka kitita cha Dola 770,000 kuidhamini Canada, hivyo kujishindia zaidi ya Dola milioni moja, sawa na faida ya Dola 231,000.

Hata hivyo, hiyo si mara ya kwanza kwake kuweka fedha nyingi kwenye kamari ya kubeti. Wakati wa fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2022, aliliwa Dola 837,000.

Kama itakumbukwa, aliingia chaka baada ya kuidhamini Ufaransa akiamini ingeifunga Argentina ya akina Lionel Messi katika mchezo wa fainali.

Endapo mambo yangekwenda kama alivyobashiri, kwa maana ya Argentina kushinda, angejiondokea na kitita cha Dola milioni 2.26.

Nyota huyo wa muziki ameshatumia zaidi ya Dola bilioni moja kubeti na kucheza kamari mbalimbali za casino tangu mwaka 2021.

Kati ya majaribio 85 aliyofanya kwenye kubeti, ameshinda 31 (36.5) na kupoteza 54. Hali iliwahi kuwa mbaya zaidi baada ya ‘kuchana mkeka’ mara saba mfululizo na kupoteza Dola milioni 3.8.

Mbali na soka, michezo mingine ambayo Drake amekuwa akibeti zaidi ni ngumi, NBA, tenesi, na mashindano ya mbio za magari ya Formula One.

Katika michezo hiyo, soka limeonekana ‘kumpasua’ zaidi, huku fedha nyingi akipata kwenye ubashiri wa matokeo ya mapambano ya ngumi.

Related articles

Recent articles