37.6 C
New York

Halotel, Samsung wazindua huduma mikopo ya simu janja yenye vifurushi

Published:

Na Imani Nathaniel, Gazetini

Kampuni ya Mawasiliano ya Halotel Tanzania kwa kushirikiana na Samsung Electronics, imezindua huduma ya mikopo ya simu janja inayokwenda sambamba na vifurushi vya mawasiliano, hatua inayolenga kuwawezesha watanzania wengi  kumiliki simu za kisasa kwa gharama nafuu.

Uzinduzi wa huduma hiyo umefanyika leo katika Banda la Halotel kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), ambapo kampuni hizo zilisema ushirikiano huo unalenga kuongeza matumizi ya teknolojia ya kidijitali nchini kwa kurahisisha upatikanaji wa simu janja.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Halotel Tanzania, Tran Thi Thuy Dung, alisema ushirikiano huo unaonyesha dhamira ya kampuni hiyo ya kupanua huduma za kidijitali kwa kuhakikisha simu janja zinapatikana kwa bei nafuu kwa Watanzania.

Amesema kupitia mpango huo, wateja watapata fursa ya kumiliki simu janja za Samsung kwa utaratibu wa malipo ya awamu huku wakinufaika na vifurushi maalumu vya mawasiliano vya Halotel.

Kwa upande wake, Meneja wa Biashara wa Samsung Electronics Tanzania,  Daesong Ra, amesema ushirikiano huo unaendana na mkakati wa kampuni hiyo wa kupanua upatikanaji wa teknolojia nchini na kuchangia ukuaji wa uchumi wa kidijitali.

Amebainisha kuwa Samsung imejipanga kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata simu halisi za kampuni hiyo kupitia mfumo wa mikopo unaowezesha malipo ya taratibu, huku wakifurahia huduma za mawasiliano kwa gharama nafuu.

Naye, Mkurugenzi wa Biashara wa Halotel, Abdallah Salum, amesema ushirikiano huo mpya utachochea maendeleo ya sekta ya mawasiliano nchini kwa kuongeza matumizi ya huduma za kidijitali na kuwawezesha wananchi wengi zaidi kumiliki simu janja.

Amesema mpango huo pia utaimarisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano ndani na nje ya mipaka ya Tanzania kupitia teknolojia za kisasa na huduma bunifu zinazotolewa na kampuni hiyo.

Huduma hiyo mpya itawawezesha wateja wanaokidhi vigezo kumiliki simu janja za Samsung kwa malipo ya awamu, jambo linalotarajiwa kuongeza matumizi ya simu janja miongoni mwa wanafunzi, vijana, wajasiriamali na familia mbalimbali nchini.

Halotel imesema wateja wanaotembelea maduka yake nchini watapata maelezo kuhusu utaratibu wa kupata simu hizo kwa mkopo, kuona aina mbalimbali za simu za Samsung zinazopatikana pamoja na kunufaika na ofa maalumu za vifurushi vya mawasiliano.

Related articles

Recent articles