WASHINGTON DC, Marekani
INAFAHAMIKA kuwa bado uhusiano kati ya Marekani na Iran haujakaa sawa. Mataifa hayo yanaendelea kushambuliana kijeshi, licha ya makubaliano ya hivi karibuni ya kusitisha vita vyao vilivyoanza Februari 28, 2026.
Sasa, ‘bifu’ la nchi hizo halijaishia kwenye siasa, bali pia limeonekana wazi wakati wa fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea.
Iko hivi; Katibu wa Masuala ya Usalama wa Marekani, Markwayne Mullin, hajaficha hisia zake, akisema amefurahi kuona Iran ikiondoshwa kwenye mashindano hayo.
Itakumbukwa kuwa Iran iliishia hatua ya makundi baada ya kupata sare katika mechi zote tatu, ikiwamo ya mwisho dhidi ya Misri.
“Nimefurahi tu kuona wametolewa,” amesema Mullin na kuongeza: “Nimefurahia kuona hawatorudi (Marekani). Ningeweza kuimba au kucheza muziki kwa furaha niliyonayo.”
Iran imekuwa na wakati mgumu kwa kipindi chote cha ushiriki wake kwenye fainali hizo zinazofanyika Marekani, Mexico na Canada.
Awali, timu yake ilipangwa kuweka kambi Arizona, Marekani, lakini ililazimika kuondoka na kuhamia mjini Tijuana, Mexico.
Hivyo, Iran ililazimika kusafiri hadi Marekani kucheza mechi na kurudi. Ilifanya hivyo katika michezo yake yote mitatu.
Akizungumza baada ya mchezo dhidi ya Misri, ambao ndiyo ulioing’oa Iran, Mullin alisema:
“Mechi imeisha. Acha warudi hotelini katika kambi waliyokuwa (Mexico). Kule ndiko wanakofurahia.
“Haya ni makubaliano tuliyokuwa nayo na FIFA (Shirikisho la Soka la Kimataifa) hata kabla ya michuano,.
Aidha, kigogo huyo alisema nusu ya viongozi wa timu ya soka ya Iran wana uhusiano wa moja kwa moja na Jeshi la Mapinduzi ya Kiislam la nchi hiyo (IRGC).


