31.4 C
New York

Samia aisifu TPA kwa kujitegemea, yakabidhi gawio la Sh bilioni 205.53

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

Rais Samia Suluhu Hassan ameisifu Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa kufikia kiwango cha kujitegemea kifedha, akisema taasisi hiyo sasa ina uwezo wa kukopa kwa hadhi yake yenyewe ili kugharamia miradi ya maendeleo bila kuongeza mzigo wa deni la Serikali.

Kauli hiyo ameitoa leo, Juni 30, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam, mara baada ya kupokea hundi ya mfano ya Sh bilioni 201.53 ikiwa ni gawio la TPA kwa mwaka wa fedha 2025/26. Hundi hiyo ilikabidhiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya TPA, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Mstaafu Ernest Mangu, pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa.

Rais Samia amesema Serikali imekuwa ikisisitiza taasisi za umma kuacha kutegemea bajeti ya Serikali kama suluhisho la kila changamoto, badala yake zitumie mali, miradi na uimara wake wa kifedha kuvutia mitaji kupitia njia halali na zenye tija.

“Nilisisitiza kuwa taasisi zetu haziwezi kuendelea kutazama bajeti ya Serikali kama jibu la kila changamoto. Baadhi zina mali, zina miradi na zina uwezo wa kuvutia mitaji kupitia njia nyingine halali na zenye tija,” amesema.

Ameitaja TPA kuwa mfano wa taasisi iliyofanikiwa kujenga uwezo wa kifedha unaoiwezesha kukopesheka kwa jina lake, hatua ambayo alisema itasaidia kupanua miundombinu ya bandari, kuongeza huduma na kuinua ushindani wa sekta hiyo bila kuliongezea Serikali deni.

“Mamlaka ya Bandari Tanzania sasa ina uwezo wa kukopesheka. Wakachukue mikopo, watanue shughuli za bandari, waongeze huduma na walipe mikopo hiyo kwa mapato yao. Hivyo deni halitaingia kwenye deni kuu la Serikali,” amesema.

Rais Samia amesema mtazamo huo unapaswa kuigwa na taasisi nyingine za umma zenye uwezo wa kifedha, akieleza kuwa hatua hiyo itapunguza shinikizo kwa Mfuko Mkuu wa Serikali, kuongeza ufanisi wa taasisi na kuimarisha mchango wake katika kukuza uchumi wa taifa.

Awali akizungumza katika hafla hiyo, Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu amesema TPA imeendelea kuongeza maradufu mchango wake jambo ambalo linaleta matumaini makubwa ya kiuchumi.

“Namba moja tuna Mamlaka ya usimamizi wa bandari Tanzania ambao mwaka jana walichangia shilingi bilioni 181 wakiongoza na mwaka huu wamechangia shilingi bilioni 205.5 hii ni pamoja na kwamba wanatumia pesa yao nyingiwanayoipata kwenda kufanya uwekezaji na utanuzi wa moundombinu yetu,” amesema Mchechu.

Related articles

Recent articles