17.4 C
New York

Haiti: Soka lilivyorejesha tabasamu la muda katikati ya vilio, simanzi

Published:

PORT-AU-PRINCE, Haiti

HAITI ni Kisiwa kilichopo Caribbean, kikifahamika kwa hali yake mbaya ya usalama kutokana na machafuko yanayosababishwa na utitiri wa magenge ya uhalifu yaliyotapakaa katika maeneo yake mengi.

Vikundi vya waasi vimekuwa na nguvu zaidi tangu Rais Jovenel Moise alipouawa mwaka 2021, ambapo kiti chake kimebaki wazi hadi leo hii.

Kwa takwimu za Shirika la Haki za Binadamu la Amnesty International, raia zaidi ya 5,600 wamepoteza maisha kutokana na mapigano ya vikundi vya waasi katika Taifa hilo lenye watu milioni 11.5.

Kutokana na hali hiyo, timu ya soka ya Taifa ya Haiti haijaweza kucheza katika ardhi yake ya nyumbani kwa miaka yote mitano ya hivi karibuni.

Ikumbukwe, uwanja iliokuwa ikiutumia kwa michezo yake ya nyumbani, Sylvio Cator, ambao unamilikiwa na klabu ya Violette AC, ulitekwa na waasi miaka miwili iliyopita.

Hivyo basi, timu hiyo imekuwa ikicheza mechi zake za nyumbani katika nchi jirani ya Curacao iliyoko umbali wa maili 500 kutoka Haiti.

Kwamba hata kocha wao raia wa Ufaransa,  Sebastien Migne, hajawahi kukanyaga Haiti tangu alipoajiriwa na badala yake amekuwa akitumiwa video ya kila kinachoendelea katika soka la Haiti.

Mfano, alipomwita Woodensky Pierre kwenye kikosi chake, ni kwa sababu alimtazama kupitia video na si kwamba alikwenda moja kwa moja uwanjani.

Woodensky anacheza soka katika maeneo hatari zaidi kiusalama. “Ni fahari ya watu wa Haiti kwa sababu anawakilisha vipaji vingi vilivyopo katika maeneo ya hatari,” anasema mwandishi wa habari wa Haiti, Pierre Richard Midy.

TABASAMU LA MUDA

Haiti kufuzu fainali za Kombe la Dunia za mwaka, ikiwa ni mara ya kwanza tangu iliposhiriki mwaka 1974, kumeleta sura tofauti katika Kisiwa hicho, ambapo magenge ya uhalifu yameungana na raia kufurahia mafanikio hayo.

“Viongozi wote wa magenge ya uhalifu ni wapenzi wa soka. Baada ya kufuzu, niliona video zao wakisherehekea kwa kuimba na kucheza muziki kama wananchi wengine huko mitaani,” anasema Midy.

Duckens Nazon, mfungaji bora wa muda wote wa timu ya Taifa ya Haiti (mabao 44 katika mechi 80), anakumbuka hali kama hiyo ilijitokeza pia walipofika nusu fainali ya Kombe la CONCACAF mwaka 2019.

“(Waasi) walituonesha video. Ilishangaza sana. Akiwahi kuona. Waasi na raia walijimuhika mitaani kufurahia mafanikio (ya timu),” alisema.

Hata hivyo, Nazon anasema anatamani kuona hali hiyo ya amani, umoja na mshikamano ikiendelea katika maisha ya kila siku.

KILA MECHI INA MAANA KWA TAIFA

Asilimia zaidi ya 90 ya wachezaji wa kikosi cha Haiti walioko Kombe la Dunia mwaka huu walizaliwa nje ya Taifa hilo. Kati ya 26 walioitwa, wanatoka katika klabu 25 za Mataifa 15 tofauti.

Kabla ya mechi yoyote, Nazon aliyezaliwa Ufaransa, ambaye watu wa Haiti wanamtaja kuwa ni ‘mzalendo namba moja’ wa Taifa lao, amekuwa akizungumza na wachezaji.

Amekuwa akiwaelezea hali iliyopo Haiti, pia uzito wa jezi ya timu ya Taifa na umuhimu wa usindi katika kurejesha furaha kwenye nyuso za raia wa nchi hiyo.

“Tuna wachezaji wengi ambao hawajawahi kuja Haiti, hivyo kabla ya mechi kuanza, huwa nawapa uhalisia wa hapa na jukumu tulilo nalo,” amesema Nazon.

“Kila mechi tunaipa uzito mkubwa. Siyo lazima ushike silaha. Siyo lazima upambane na magenge ya uhalifu. Kuna njia nyingi za kurejesha furaha katika changamoto iliyopo,” amesema.

Kwa upande wake, Midy anamzungumzia kocha wao, Migne, ambaye alikuwa msaidizi katika benchi la timu ya Taifa ya Cameroon wakati wa fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2022 nchini Qatar.

“Ni kocha mzuri. Nikitazama mechi za Haiti, siwezi kueleza inavyocheza. Niliwahi kumuuliza, akanijibu ‘siyo mimi, ni wachezaji. Sina siri yoyote. Huwa nawaambia tu wajitoe,” anasema Midy.

Related articles

Recent articles