Na mwandishi wetu, Gazetini
AKIWA ugenini nchini Ivory Coast, bondia wa uzito wa Middle nchini, Hassan Mwakinyo, alishindwa kutwaa ubingwa wa dunia wa IBO baada ya kupigiwa kwa KO ya raundi ya tisa na mwenyeji wake, Michel Soro.
Mwakinyo ‘Champez’, aliingia katika pambano hilo lililopigwa katika Ukumbi wa Parc Des Expositions mjini Abidjan akiwa na rekodi nzuri dhidi ya wapinzani wake wa awali.
Alimkabili Soro akiwa na rekodi ya kushinda mapambano 25 (18 kwa KO) na kupoteza matatu pekee, hivyo kuwa na matarajio makubwa ya kuibuka na ushindi mbele ya bondia huyo mwenye uraia-pacha wa Ivory Coast na Ufaransa.
Kabla ya kuvaana na Mwakinyo, Soro mwenye umri wa miaka 39, alikuwa na rekodi ya kucheza mapambano 44, akishinda 38, sare mbili na kupigwa mara nne.
Hivyo, sasa amefikisha apambano yake 45, akishinda 39 (28 kwa KO), sare mbili na kupigwa mara nne pekee (moja kwa TKO).
Mara yake ya mwisho kupanda ulingoni kabla ya kuvaana na Mwakinyo ilikuwa Oktoba, 2025, ambapo alimdunda Evander Castillo. Hajapoteza pambano tangu Mei, 2023, alipopigwa na Magomed Kurbarnov.
Alizaliwa Oktoba 30, 1987. Alianza ngumi za kulipwa mwaka 2008, ambapo alishinda mapambano 18 mfululizo kabla ya kupigwa kwa mara ya kwanza Mei, 2012 na Zaurbek Baysangurov.
Baada ya kichapo hicho, ilipita miaka mitano, kabla ya kupigwa tena Julai, 2017, safari hii akitandikwa na Brian Carlos Castano.
Novemba, 2020, Jarida maarufu la mchezo wa masumbwi la The Ring lilimtaja Soro kushika nafasi ya nane katika orodha ya mabondia bora wa sasa wa uzito wa super middle.
Desemba, 2021, Soro alionja kichapo chake cha tatu, alipopigwa na Israil Madrimov, kabla ya kile cha mwisho mbele ya Magomed Kurbarnov (Mei, 2023).


