BEIRUT, Lebanon
HIVI karibuni, vikosi vya jeshi la Israel viliitaja kuwa ni mafanikio makubwa hatua ya kuiteka Ngome ya Beaufort iliyoko Lebanon.
Kwamba ni hatua kubwa katika vita vyao na wapiganaji wa kundi la kigaidi la Hezbollah huko Kusini mwa nchi hiyo.
Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, alisema: “Wanajeshi wetu wa kihistoria wameishikilia kwa mara nyingine Ngome ya Beaufort na itaendelea kuwa sehemu yake ya usalama nchini Lebanon.
Taarifa za kuishikilia Ngome hiyo zinakuja wakati huu wanajeshi wa Israel wakiendelea kushambuliana, licha ya pande mbili hizo kukubaliana kusitisha vita.
Swali ni je; Ngome ya Beaufort ni nini? Ina umuhimu gani kwa pande zote mbili (Israel na Lebanon)? Na je, ni pigo kwa Hezbollah?
Ngome ya Beaufort au Qalaat al-Shaqif kama inavyojulikana kwa lugha ya Kiarabu, ilijengwa miaka 900 iliyopita (karne ya 12) huko Kusini mwa Lebanon, ikiwa na urefu wa futi 2,300.
Kwa miaka ya hivi karibuni, wapiganaji wa Palestina waliitumia Ngome hiyo kama kambi yao ya kijeshi, kabla ya Israel kuikamata mwaka 1982 na kuiachia mwaka 2000.
Ngome hiyo iliyoko Nabatieh, ambao ni Mji wa tano kwa ukubwa nchini Lebanon, imekuwa muhimu na eneo la kimkakati katika masuala ya kiusalama.
Kwa Israel, kuiteka Ngome hiyo kunaipa nafasi ya wanajeshi wake kuimarisha ulinzi katika eneo lao la Kaskazini linalopakana na Kusini mwa Lebanon.
Ifahamike, kwa miaka mingi, wapiganaji wa Hezbollah wamekuwa walitumia Ngome hiyo kutekeleza mashambulizi yake katika maeneo mbalimbali nchini Israel.
Hivyo, kwa mujibu wa wachambuzi wa siasa za Ukanda huo, Israel kuingia Beaufort kunaipa nafasi ya kudhibiti vijiji na maeneo yote yaliyoko Nabatieh, Mji iliyoko Ngome hiyo.
Pia, kwa kushika Ngome hiyo, wachambuzi wanaona Israel inapata nafasi kubwa zaidi ya kusonga mbele katika kuyafikia machimbo ya Hezbollah huko Kusini mwa Lebanon.
Kusini mwa Lebanon kumekuwa na fukuto kubwa la vita kati ya vikosi vya Israel na wapiganaji wa Hezbollah, ambalo jumuhiya za kimataifa zimekuwa likilitaja kuwa ni kundi la kigaidi.
Wizara ya Afya ya Lebanon inaeleza kuwa watu zaidi ya 3,412 wameuawa na wengine 10,269 kujeruhiwa na mashambulizi ya Israel kwa kipindi kifupi cha miezi mitatu iliyopita.
Mji wa Nabatieh ndiyo kitovu cha mapigano hayo na Israel imeiteka Ngome ya Beaufort baada ya shambulizi lililosababisha vifo vya watu 12 na majeruhi 35.
Kwa sasa, Israel inadhibiti eneo kubwa (kimoleta za mraba 2,000) nchini Lebanon na huenda kuiteka Ngome ya Beaufort kukaiongezea nguvu zaidi, kama alivyosema Waziri Mkuu wake, Benjamin Netanyahu.


