Na Winfrida Mtoi, Gazetini
BEKI wa timu ya Taifa (Taifa Stars), Nickson Kibabage amesema kitendo cha vijana wa timu ya Serengeti Boys kufika fainali ya AFCON – U17 na kiwango walichoonesha ni fursa ya kwenda kucheza soka la kulipwa katika mataifa makubwa.
Serengeti Boys inatarajia kushuka dimbani kesho kuchuana na Senegar katika mchezo wa fainali wa michuano hiyo katika Uwanja wa Moulay Hassan, Rabat nchini Morocco.
Kibabage ambaye alikuwa miongoni mwa wachezaji waliunda kikosi cha Serengeti Boys iliyofanya vizuri mwaka 2016, ametoa kauli hiyo leo Juni 1, 2026, akiwapongeza vijana hao kwa kuandika historia ya pekee.
Amesema ni jambo la kupongeza kwa sababu Tanzania haijawahi kucheza fainali hizo, akiamini Serengeti Boys ina uwezo wa kutwaa ubingwa wa michuano hiyo kutokana na kiwango walichoonesha katika michezo yote.
“Kwanza tunawapongeza kwa hatua walitofikia, ni jambo la kihistoria na kesho wanakwenda kukamilisha historia. Ni moja jambo kubwa sana kwa nchi yetu Tanzania, haijawahi kutokea hususani kwa timu za vijana kufika hatua hii”, amebainisha.


