17.4 C
New York

Tume ya Taifa ya Mipango yaongoza mjadala wa Afrika kujitegemea kiuchumi

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

TUME ya Taifa ya Mipango imeongoza mjadala wa wanazuoni na wadau mbalimbali kuhusu mustakabali wa maendeleo na kujitegemea kiuchumi kwa nchi za Afrika katika Kongamano la 17 la Kigoda cha Kiprofesa cha Mwalimu Julius Nyerere lililofanyika Mei 29, 2026 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mjadala huo uliongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, ambaye amesema Afrika inapaswa kuachana na utegemezi wa kuuza malighafi nje huku ikiendelea kuagiza bidhaa zilizoongezwa thamani.

“Afrika haitakiwi kuuza malighafi nje huku ikiagiza bidhaa. Mustakabali wetu unategemea ukuaji wa viwanda, ushirikiano wa kikanda, mabadiliko ya kidijitali na uwekezaji kwa vijana wetu,” amesema Prof. Mkumbo.

Amesema Tume ya Taifa ya Mipango itaendelea kuwa mstari wa mbele kutafuta njia za kuiwezesha Tanzania kujenga uchumi imara unaojitegemea na wenye uwezo wa kushindana kimataifa kupitia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dk. Tausi Kida (kulia) akifafanua jambo akati wa Mjadala huo, kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dk. Tausi Kida, amesema Dira 2050 inalenga kujenga taifa lenye ushindani wa kiuchumi, ubunifu na maendeleo jumuishi.

Ameeleza kuwa utekelezaji wa dira hiyo utazingatia kuongeza tija katika sekta za kilimo na viwanda, kuboresha miundombinu ya nishati na usafiri pamoja na kuimarisha mifumo ya utendaji.

Wanazuoni walioshiriki mjadala huo walijadiliana kuhusu nafasi ya Afrika katika uchumi wa dunia, maendeleo ya teknolojia na umuhimu wa bara hilo kujitegemea kiuchumi.

Related articles

Recent articles