LONDON, Uingereza
WASHIKA Bunduki wa London, Arsenal, wameanza kuifukuzia saini ya mashambuliaji wa Bayer Leverkusen ya Bundesliga, Christian Kofane.
Arsenal wako kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya England wakiwa na pointi 70 katika mechi zao 31.
Ni kwa maana hiyo, wameizidi pointi tisa Manchester City inayoshika nafasi ya pili, licha ya kwamba Arsenal wana michezo mingi zaidi.
Vijana hao wa Emirates wana mabao 61 ya kufunga lakini kocha wao, Mikel Arteta, hajaonesha kuridhishwa na idadi hiyo.
Viktor Gyokeres, licha ya usajili wake wa bei mbaya, amefunga mabao 11 pekee kwenye Ligi, wakati Gabriel Jesus ameingia kambani mara mbili.
Kofane (19), ambaye alitua Leverkusen mwaka jana akitokea Albacete, ameshazifumania nyavu mara tano na kutoa ‘asisti’ tatu katika mechi 14 za Bundesliga msimu huu.
Kwa upande wao, Leverkusen wanataka Pauni milioni 61 ili kumwachia nyota wao huyo ambaye pia anawindwa na Real Madrid na Manchester City.


