NEW YORK, Marekani
TAHARUKI imezuka juu ya hali ya afya ya rapa maarufu wa Marekani, Lil Wayne, ambaye inaelezwa kuwa staa huyo hayuko sawa.
Hivi karibuni, ziliibuka ripoti kuwa mwanamuziki huyo anasumbuliwa na ugonjwa hatari wa saratani ya ubongo, ingawa si yeye wala familia yake iliyothibitisha.
Hata hivyo, si tu hata vyombo vya habari vikubwa havijathibitisha, bali pia hii si mara ya kwanza kwa Wayne kuhusishwa na magonjwa.

Wakati fulani, kama itakumbukwa, zilikuwepo taarifa zilizodai kuwa rapa huyo mzaliwa wa New Orleans ana saratani ya mapafu.
Aidha, hivi karibuni jina lake lilishika vyombo vya habari baada ya kile kilichoelezwa kuwa nyumba yake ya zamani iliyoko mjini Miami imeuzwa.
Ni nyumba yenye vyumba vya kulala saba, ikiwa na ukubwa wa meta za mraba 10,632, ambayo Wayne alikuwa akiishi katika miaka ya 2010.
Mjengo huo aliuuza kwa Dola za Marekani milioni 22 na sasa imeuzwa kwa Dola milioni 33. Uko jirani na nyumba ya mmiliki wa Google, Sergey Brin.
Kuhusu hali yake ya kiafya, kwa sasa Wayne ambaye jina lake halisi ni Dwayne Carter hajathibitisha juu ya taarifa za ugonjwa wa saratani ya ubongo.
Lakini, wengi watakumbuka mahojiano yake ya mwaka 2023. Wayne alikiri kusumbuliwa na tatizo la kupoteza kumbukumbu, akisema amekuwa akisahau hata nyimbo zake.
Aliwashangaza wengi aliposema hata albamu yake kubwa zaidi, ‘Tha Carter III’, hajui iliingia sokoni mwaka gani. Iliachiwa mwaka 2008.


