MANCHESTER, Uingereza
KLABU ya Manchester United italazimika kuweka mezani kitita cha Pauni milioni 60.5 ili kukamilisha usajili wa kiungo wa Newcastle United, Bruno Guimaraes.
Man United imekuwa kwenye mawindo ya Mbrazil huyo na ripoti zinaeleza kuwa Newcastle wako mbioni kumpoteza mwishoni mwa msimu huu.
Guimaraes ana mkataba utakaofikia ukomo mwaka 2028 lakini inaelezwa kuwa nyota huyo hana mpango wa kuumaliza akiwa klabuni hapo.
Tangu msimu huu uanze, staa huyo ameshaingia kambani mara tisa na kutoa ‘asisti’ saba katika mechi 35 za mashindano mbalimbali.
Aidha, takwimu za jumla zinaonesha kuwa amechangia mabao 31 na asisti 31 katika mechi 189 alizocheza tangu asajiliwe akitokea Lyon mwaka 2022.
Kwa upande wao, Man United wanamtaka Guimaraes wakiamini anatosha kuvaa viatu vya Casemiro aliyetangaza kuwa huu ni msimu wake wa mwisho Old Trafford.


