18.5 C
New York

WHO yathibitisha shambulio jingine la hospitali Sudan, watu 64 wafariki

Published:

DARFUR, Sudan

SHIRIKA la Afya Duniani (WHO) limethibitisha kutokea kwa shambulio jingine dhidi ya huduma za afya nchini Sudan, safari hii likilenga Hospitali ya Kufundishia ya Al Deain iliyopo mji mkuu wa jimbo la Darfur Mashariki.

Akitoa taarifa kupitia mtandao wa kijamii wa X, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk. Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema shambulio hilo limesababisha vifo vya watu takribani 64 na kujeruhi wengine 89.

“Waliofariki ni pamoja na watoto 13, wauguzi wawili wanawake, daktari mmoja na wagonjwa kadhaa. Wengine walioumia ni pamoja na wahudumu wanane wa afya,” amesema Dk. Tedros.

Kwa mujibu wa WHO, shambulio hilo limeharibu vibaya idara za watoto, wazazi na dharura za hospitali hiyo, hali iliyosababisha kusitishwa kwa huduma muhimu za matibabu katika kituo hicho.

Dk. Tedros amesema tukio hilo linaongeza idadi ya vifo vinavyotokana na mashambulizi dhidi ya vituo vya afya tangu kuanza kwa vita nchini Sudan, ambapo hadi sasa zaidi ya watu 2,000 wamepoteza maisha katika mashambulizi 213 yaliyothibitishwa.

Aidha, zaidi ya watu 720 wamejeruhiwa katika mashambulizi hayo ndani ya kipindi cha takribani miaka mitatu ya mzozo huo.

“Mashambulizi dhidi ya huduma za afya yana athari kubwa kwa jamii zinazohitaji huduma hizo kwa dharura,” ameonya.

WHO imesema inaendelea kushirikiana na wadau wa ndani kuimarisha huduma katika vituo vingine, huku Dk. Tedros akitoa wito wa kusitishwa kwa mapigano akisisitiza, “Huduma za afya hazipaswi kuwa shabaha ya mashambulizi. Amani ndiyo tiba bora.”

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img