LOS ANGELES, Marekani
PESA siyo tatizo. Kwa miaka aliyofanya kazi ya muziki, Chris Brown ameweza kujikusanyia utajiri wa Dola za Marekani milioni 50, huku vyanzo vingine vikisema ameshafikisha Dola milioni 80.
Kufikia Januari, 2026, alikuwa ameingia mara 54 kwenye ‘Top 40’ ya chati za Billboard Hot 100. Pia, alishaingia mara 17 kwenye ‘Top 10’ ya chati hizo.
Wakati huo huo, bado anashika nafasi ya 10 kwenye orodha ya wasanii wenye mauzo makubwa nchini Marekani kwa upande wa majukwaa ya kidigitali.
Huo ni upande mmoja. Nje ya kazi, Brown anafahamika kuwa ni mmoja ya wasanii watukutu, ambao kwao ni kawaida kuingia na kutoka katika vituo vya polisi.
Mei 15, 2025, alikamatwa akiwa katika chumba cha hoteli moja mjini Salford, Uingereza. Alikamatwa kwa kosa la mwaka 2023, ambapo alimpiga chupa ya kichwa promota aitwaye Abraham Diaw wakiwa klabu ya usiku jijini London.
Halikuwa tukio pekee. Miongoni mwa matukio yake ni lile la mwaka 2024, ambapo Brown alifunguliwa mashitaka mjini Texas, akitajwa kushirikiana na watu wake kuwapiga watu wanne baada ya shoo yake katika Uwanja wa Dickies Arena.
Pia, mwaka 2021, mwanamke mmoja alimshitaki Brown kwa kosa la kumpiga, kabla ya kesi yake na Drake waliposhutumiwa kwa kuiba vionjo vya wimbo ‘I Love Your Dress’ katika kolabo yao ya ‘No Guidance’.
Aidha, mwaka 2019, supastaa huyo wa muziki wa R&B alikamatwa jijini Paris, Ufaransa, kwa tuhuma za kubaka na kukutwa na dawa za kulevya.
Kwa upande mwingine, mwaka 2018, mawakala wa wanyamapori walimpokonya ngedere wake baada ya kubaini alikuwa akimfuga pasi na kufuata sheria.
Ni mwaka huo pia, alitajwa kumfanya unyanyasaji wa kingono binti aitwaye Jane Doe aliyekuwa mmoja ya wageni waliohudhuria ‘party’ iliyofanyika nyumbani kwa Brown.

Mwaka 2017, Brown alitakiwa na Mahakama kukaa mbali na aliyekuwa mpenzi wake, Karrueche Tran. Ni baada ya bibiye huyo kushitaki kuwa jamaa amekuwa akimtishia maisha kwa muda mrefu. Tukio hilo lilifuatiwa na lile la Brown kumpiga ngumi mpiga picha.
Mwaka 2016, moja ya matukio yake ni lile la kukamatwa na kuachiwa kwa dhamana baada ya mwanamke mmoja kuripoti polisi kuwa staa huyo amemtishia maisha mjini Los Angeles. Kwa mujibu wa mwanamitindo huyo, Brown alitishia kumpiga bastola baada ya kutupiana maneno.
Mei 5, 2015, aliripotiwa kupigana na mwanaume mmoja walipokutana kwenye mechi ya kikapu jijini Las Vegas. Polisi walieleza kuwa Brown hakuwa peke yake, alishirikiana na wenzake kumsababishia majeraha mtu huyo.
Julai 15, 2013, Brown alifunguliwa mashitaka kwa kosa la kugonga mtu kwa gari na kisha kukimbia. Hiyo ilitokea Los Angeles lakini kesi ilifutwa baada ya pande mbili (Brown na aliyeshitaki) kukubaliana.
Miezi mitatu baadaye, yeye na mlinzi wake walishitakiwa kwa kumpiga hadi kumvunja pua shabiki aliyetaka kupiga naye picha nje ya hoteli moja mjini Washington DC.
Mwaka huo pia, Januari 27, 2013, Brown alimpiga ngumi mwanamuziki mwenzake, Frank Ocean, chanzo cha ugomvi kikiwa ni kugombea eneo la kuegesha gari walipokutana nje ya studio huko California.
Juni 14, 2012, Brown aliripotiwa kutaka kupigana na staa mwenzake wa muziki, Drake, walipokutana kwenye ‘bata’ nyakati za usiku. Rihanna akatajwa kuwa ndiyo chanzo kwa kuwa Drake naye aliwahi kutoka naye.
Tukio hilo lilifuatiwa na lile la Machi 22, 2012, ambapo mwanamuziki huyo alimrushia kiti mtangazaji wa kipindi cha televisheni cha ‘Good Morning America’, Robin Roberts, baada ya kuulizwa juu ya tukio la kumpiga Rihanna.
Hata hivyo, tukio kubwa zaidi ni lile la Februari, 2009, wakati huo Brown akiwa kijana wa umri wa miaka 19. Alitikisa vyombo vya habari kwa tukio lake la kumtembezea kichapo mpenzi wake wakati huo, Rihanna.


