RABAT, Morocco
DROO ya hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho imechezeshwa leo Februari 17, 2026 mjini Rabat.
Je, droo hiyo iliyosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka Afrika imezikutanisha timu zip? Endelea kusoma …
Kombe la Shirikisho

Kwa upande wa Kombe la Shirikisho, Al Masry ya Misri imekutanishwa na wakali wa Algeria, CR Belouizdad.
Mechi nyingine ni ile ya Olympique Club de Safi dhidi ya wenzao wa Morocco, Wydad AC, wakati AS Otoho (Congo) wataikabili Zamalek.
Wakati huo huo, AS Maniema Union wataisaka tiketi ya kucheza nusu fainali kwa kuivaa USM Alger.
Kwa mujibu wa ratiba ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), mechi za hatua hiyo ya robo fainali zitaanza kuchezwa Marchi 15, 2026.
Timu itakayoshinda kwa matokeo ya jumla (baada ya mechi mbili) atajiondokea na kitita cha Dola za Marekani 550,000, huku bingwa wa mashindano akibeba Dola 2,000,000.
Ligi ya Mabingwa Afrika
Kwa Ligi ya Mabingwa, RS Berkane ya Morocco imepangwa kukutana ana kwa ana na wakongwe wa soka la Sudan, Al Hilal.
Pia, kuna robo fainali nyingine itakayozikutanisha Esperance ya Tunisia na mabingwa mara nyingi wa Ligi ya Mabingwa, Al Ahly.
Hii ni kama marudio ya fainali ya Ligi ya Mabingwa mwaka 2024, ambapo Al Ahly walitwaa ubingwa.
Aidha, wababe wa soka la Afrika Kusini, Mamelodi Sundowns, wao wana kibarua cha kuivaa Stade Malien ya Mali.
AS FAR ya Morocco wana robo fainali yao ngumu mbele ya matajiri wa soka la Misri, Pyramids, ambao wanatetea taji walilobeba msimu uliopita.
Mechi za robo fainali zinatarajiwa kuanza kuchezwa Marchi 13, 2026, huku zile za marudiano zikiwa zimepangiwa wiki moja baadaye.
Mshindi wa robo fainali atajinyakulia Dola 900,000, wakati bingwa wa mashindano ya msimu huu akilamba Dola 4,000,000.


