Na mwandishi wetu, Gazetini
MWAKA 2025 tayari umemalizika, huku ukiacha kumbukumhu nzuri katika tasnia ya burudani duniani kote.
Kwa upande mwingine, kumbukumhu hizo ni pamoja na mastaa wakubwa nchini Marekani na maeneo mengine walioamua kuachana na ukapera na kuingia kwenye ndoa.
Selena Gomez
Baada ya usiri mkubwa tangu alipovishwa pete ya uchumba na Beeny Blanco, staa hiyo wa muziki, ambaye aliwahi kuwa mpenzi wa Justin Bieber, aliolewa Septemba, mwaka jana.
Sherehe ya harusi yao ilifanyika mjini California na kuhudhuriwa na mastaa wengi, wakiwamo Taylor Swift, Ed Sheeran, Steve Martin na Martin Short.
Patrick Schwarzenegger
Ni mwigizaji na mtoto wa mkongwe wa filamu za Hollywood, Arnold Schwarzenegger. Patrick alimuoa mpenzi wake wa siku nyingi, Abby Champion.
Ndoa yao ilifungwa Septemba 6, mwaka jana. “Siamini kama limepita. Ilikuwa kama ndoto. Nasubiri kwa hamu kuanza maisha mapya na Patrick,” alisema Abby.
Mel B
Mbali ya kuwa staa wa muziki nchini Marekani, pia ni mmoja ya wasimamizi wa Shindano maarufu la vipaji la ‘Americas Got Talent’.
Aliolewa na mbunifu wa urembo wa nywele, Rory McPhee, na ndoa yao ya kifahari ilifungwa Julai 5, mwaka jana, mjini London, Uingereza.
Davido
Nyota wa muziki nchini Nigeria. Alimuoa mpenzi wake wa miaka mingi, Chioma Adeleke, na ndoa ilifungwa nje ya Taifa hilo la Afrika ya Magharibi.
Ilikuwa ni Agosti 10, mwaka jana, huko Miami, Marekani, ambapo harusi yao ilihudhuriwa na mastaa wengi.
Priscilla Ojo
Huyo ni binti wa staa wa soko la filamu za Nigeria (Nollywood), Iyabo Ojo. Priscilla aliolewa na mwanamuziki wa Tanzania, Juma Jux, ndoa yao ikifungwa Aprili, mwaka jana.
Ni ndoa iliyokuwa na sherehe tatu tofauti. Moja ilifanyika Tanzania, nyingine ikawa Yoruba, kabla ya ile ya Lagos.
Mr Eazi
Supastaa wa muziki wa Afrobeat nchini Nigeria. Alimuoa Temi Otedola, ambaye si tu ni mwigizaji, bali pia ni binti wa bilionea Femi Otedola.
Ndoa yao ilikuwa na sherehe tatu za kifahari. Moja ilifanyika Mei, mwaka jana, mjini Monaco, nyingine ikawa Julai mjini Dubai, kisha ikafuta ya Agosti nchini Iceland.


