LAGOS, Nigeria
WATOTO wengine 130 waliokuwa wametekwa na waasi mwezi uliopita nchini Nigeria wameachiwa na kuungana na familia zao.
Ikumbukwe, watoto hao ni miongoni mwa wanafunzi 315 waliotekwa wakati waasi walipovamia Shule ya Kikatoliki katika Kijiji cha Papiri ndani ya Jimbo la Niger.
Kwa sasa, idadi ya walioachiwa imefikia 250 baada ya wale 100 walioachiwa Desemba 8, mwaka huu. Wengine 50 waliwatoroka waasi na kurudi nyumbani.
Msaidizi wa Rais wa Nigeria, Bola Tinubu, amedai kuwa kurejea kwa watoto hao wa sasa ni matokeo ya operesheni ya kijeshi.
Kwa miaka ya hivi karibuni, hali ya usalama nchini humo imekuwa ya kutilia shaka, kama ambavyo gazeti la Puch lilivyoripoti hivi karibuni.
Katika kile kilichoelezwa na Gazeti hilo, tayari watu 490 wameshatekwa na waasi ndani ya wiki mbili tu zilizopita.


