9.8 C
New York

Mo’ Dewji bado yumo, Dangote aongoza tena utajiri Afrika

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

RIPOTI mpya ya jarida maarufu la Forbes inamtaja mfanyabiashara wa Tanzania, Mohamed ‘Mo’ Dewji, kuwa nafasi ya 12 katika orodha ya mabilionea barani Afrika.

Wakati huyo huo, mfanyabiashara wa Nigeria, Aliko Dangote, anaongoza kwa ukwasi barani Afrika baada ya kuongeza utajiri wake kutoka Dola bilioni 23.9 aliokuwa nao Machi, mwaka huu, hadi Dola bilioni 25.6.

Kwa mujibu wa Forbes, bado Dewji anabaki nafasi ya 12 baada ya kulinda utajiri wake wa Dola za Marekani bilioni 2.2 (Sh trilioni 5.8 za Tanzania).

Ni utajiri aliokuwa nao katika ripoti ya Machi 29, mwaka huu, hiyo ikitokana na mafanikio ya uwekezaji wake kwenye viwanda vya nguo, unga wa ngano na sembe, mafuta ya kupikia, sabuni, sukari na vinywaji.

Hata hivyo, Dewji anaendelea kuwa bilionea mwenye umri mdogo zaidi Afrika, pia akiwa ndiye anayeongoza kwa utajiri kwa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Kwa upande wa Dangote, huu ni mwaka wa 14 mfululizo akiwa kinara, ingawa orodha hiyo ya Forbes imetawaliwa zaidi na mabilionea kutoka nchi za Nigeria, Afrika Kusini na Misri.

Johann Rupert mwenye utajiri wa Dola bilioni 16.2 anashika nafasi ya pili, akifuatiwa na Nicky Oppenheimer (Dola bilioni 10.5).

Aidha, Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Patrice Motsepe, anashika nafasi ya tisa katika orodha hiyo akiwa na utajiri unaokadiriwa kufikia Dola bilioni 3.6.

Nafasi ya nne ni Nassef Sawiris (Dola bilioni 8.4), akifuatiwa na Mike Adenuga (Dola bilioni 6.3), Abdulsamad Rabiu (Dola bilioni 8.5), Naguib Sawiris (Dola bilioni 5), Koos Bekker (Dola bilioni 3.8), na Motsepe (Dola bilioni 3.6), na Mohamed Mansour (Dola bilioni 3.4).

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img