22.2 C
New York

JAB yawatambua wanahabari wakongwe

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imeanzisha utaratibu wa kutoa ithibati ya uanachama wa maisha kwa waandishi wa habari waliokuwa na umri wa miaka 50 au zaidi mwaka 2016, hatua inayolenga kutambua mchango wa wanahabari wakongwe waliotumikia taaluma hiyo kwa muda mrefu na wanaokidhi vigezo vya kisheria.

Sambamba na hatua hiyo, JAB imeongeza kasi ya uhakiki wa sifa za waandishi wa habari nchini ili kuhakikisha taaluma ya habari inaendelea kufanywa na watu wenye sifa zinazotakiwa kwa mujibu wa sheria.

Akizungumza kwenye maonyesho ya sabsaba, 2026, katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Mkurugenzi wa JAB, Patrick Kipangula, alisema zoezi la uhakiki tayari limefanyika katika mikoa ya Dodoma, Iringa na Morogoro na litaendelea katika mikoa mingine nchini.

Alisema JAB inahakiki sifa za kitaaluma za kila mwandishi wa habari ili kujiridhisha kuwa amehitimu katika taasisi zinazotambuliwa na anamiliki vyeti vinavyokubalika kisheria.

“Tunataka kujiridhisha kuwa watu wote wanaofanya kazi katika sekta ya habari wanakidhi masharti yaliyowekwa na sheria. Kila mwandishi anayefanya kazi lazima awe na sifa zinazotakiwa,” amesema Kipangula.

Alifafanua kuwa waandishi waliowahi kuondolewa kwenye orodha ya waliothibitishwa hawatarejeshwa hadi watakapothibitisha kuwa wanatimiza vigezo vilivyowekwa.

Aidha, alisema maamuzi ya ithibati hufanywa kwa kuzingatia uhakiki wa nyaraka rasmi, si taarifa zinazotolewa kupitia mitandao ya kijamii.

“Mtu asiye na sifa zinazotakiwa hawezi kurejea kufanya kazi ya uandishi wa habari au utangazaji hadi atakapokidhi masharti ya kisheria,” alisema.

Kipangula aliongeza kuwa JAB inaendelea pia kuhakiki vyeti vya wahitimu wa ndani na nje ya nchi kuanzia ngazi ya stashahada, ili kuhakikisha vinaendana na viwango vya elimu vinavyotambuliwa nchini na hivyo kulinda hadhi na weledi wa taaluma ya uandishi wa habari Tanzania.

Related articles

Recent articles